Dodoma. Mbunge wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka amemtuhumu Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Judith Nguli kwa kuwaweka ndani watumishi wa halmashauri bila kufuata utaratibu.
Alidai katika kipindi cha mwaka mmoja amewaweka ndani watumishi 20, hivyo kudhoofisha utendaji.
Hata hivyo, Judith alisema anafanya kazi kwa kuzingatia taratibu, kanuni, miongozo na sheria na kuwa hakuna mtu yeyote aliyeonewa katika utekelezaji wa majukumu yake ya ukuu wa wilaya.
“Sina uchizi, nafanya kazi vizuri tu, bahati nzuri sana nimefundisha miaka 14, Sheria ya Utumishi wa Umma naifahamu sana. Najua ninachofanya lakini kuna wakati ni lazima niitumie hii sheria (ya kuwaweka ndani watu kwa saa 24) bila hivyo mambo hayaendi,” alisema Judith.
Akizungumza jana wakati akichangia bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/23, Kuchauka alisema namna nzuri ya kwenda kusimamia bajeti hiyo ni kuwa na watu waadilifu wanaofuata misingi ya utawala bora.
Alisema ili kuwapata watu hao ni Serikali kujikita katika kuimarisha vyuo vya utawala bora nchini na kuhakikisha watumishi wanapata mafunzo wanapokuwepo kazini.
Kuchauka alisema ni jambo jema kuwaamini vijana, lakini walio wengi bado hawajapita katika vyuo vya utumishi wa umma na hivyo ni muhimu kuwapeleka kwenye mafunzo na semina za kujua majukumu yao.
“Leo hii wako Ma-DC (wakuu wa wilaya), wako Ma- RC (wakuu wa mikoa) ziko sheria zinazowalinda na zipo sheria ambazo wanazitumia kwa kutozijua ama kwa makusudi. Iko sheria moja ya saa 24 kwa Ma-DC na saa 48 kwa wakuu wa mikoa. Matumizi ya sheria hii imekuwa ikiwaumiza sana wananchi,” alisema.
Alisema aliyekuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika aliwaeleza bungeni kuwa wanaopaswa kuwekwa ndani na viongozi hao, ni wale ambao kukaa kwao nje kutahatarisha usalama wao au kuwepo kwao nje kutahatarisha usalama wa jamii.
Kuchauka alisema viongozi hao wakishawaweka ndani watu wanatakiwa kwenda kuandika katika kitabu cha polisi sababu za kuwashikilia kwa muda huo na kesho yake anatakiwa kufikishwa mahakamani.
“Katika wilaya yangu ya Liwale ninaye DC ndani ya mwaka mmoja tayari ameshaweka ndani watu 20. Kati ya hao 20 hakuna hata mmoja aliyefunguliwa mashtaka mahakamani,” alisema.
Kuchauka aliwataja baadhi ya watu waliowekwa ndani na mkuu huyo wa wilaya kuwa ni Diwani wa kata ya Nang’ano Abdallah Lilombe, mtendaji wa kata hiyo Erick Mpinga, mtendaji wa kijiji Neema Kibasi, mganga mfawidhi wa zahanati ya Ngongowele.
Wengine aliowataja kwa vyeo tu ni ofisa maliasili kata ya Kimambi, ofisa mifugo wa wilaya, ofisa mifugo wa kata, ofisa manunuzi wa wilaya, mwenyekiti wa Chama cha Ushirika (Amcos), Katibu wa Amcos, dereva na utingo.
Kuchauka alisema kati ya hao hakuna aliyepelekwa mahakamani, hivyo kusababisha utendaji katika halmashauri hiyo kushushwa.
“Leo halmashauri ime-paralyse (haifanyi vizuri) hakuna anayefanya kazi kwa kujiamini, watu wanasubiri maelekezo, unamweka ndani mganga mfawidhi kwa kosa kwamba jengo limejengwa vibaya, yeye sio engineer (mhandisi), wala si ofisa manunuzi halafu ukimweka ndani humpeleki mahakamani inasaidia nini?” alihoji.
Alitaka wateule hao kupelekwa katika vyuo ili wakasome utawala bora na wapewe miongozo waisome vizuri wajue mipaka yao ni ipi katika uongozi.
“Nimelisema hili kwa sababu halmashauri ya Liwale hakuna anayefanya kazi, ime-paralyse kila mtu anasubiri kuwekwa ndani tu. Linakwenda kuondoa maana ya utawala bora. Kama diwani ameshawekwa ndani basi na mbunge anaweza kuwekwa ndani,” alisema.
DC afunguka
Alipoulizwa na Mwananchi, Judith alisema maamuzi yote yaliyosababisha kuwekwa ndani kwa watumishi hao, yalifanywa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na hivyo Kuchauka alipaswa kuituhumu kamati nzima na si yeye mwenyewe.
Alitaja baadhi ya sababu zilizofanya watumishi hao kuwekwa ndani kuwa ni pamoja na ubadhirifu na kukiuka maagizo ya viongozi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, jambo ambalo ni dharau.
“Mimi siwezi kuchukua hatua nikiwa nimelala ndani eti kamata weka ndani, hiyo haipo. Sina uchizi huo…Lazima tukamate tuweke ndani wanaoonekana kesi zao za kwenda Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) waende huko,” alisema.
Alisema hadi anafikia hatua ya kumchukulia hatua mtu ni kwamba ameshamuonya mara nyingi lakini hataki kulifanya jambo kama aliloagizwa, na kwamba kabla ya kumweka ndani mtu yeyote ni lazima amwambie mhusika, jambo ambalo linamfanya kuchukuliwa hatua hiyo.
“Nafanya kazi vizuri tu, bahati nzuri sana nimefundisha miaka 14, Sheria ya Utumishi wa Umma naifahamu sana. Najua ninachofanya lakini kuna wakati inabidi niitumie hii sheria, bila hivyo mambo hayaendi,” alisema.
Aliwataka watumishi na madiwani kufanya kazi zao kwa kuzingatia taratibu, sheria, miongozo ya majukumu yao.