Mbunge Ataka Jina la Hifadhi ya Burigi Chato Libadilishwe





 
Mwanza. Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa ameiomba serikali kubadilisha jina la Hifadhi ya Burigi-Chato kuwa Burigi ili kusadifu jina la ilipo hifadhi hiyo.

Hifadhi hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2019 kwa kuunganisha mapori ya akiba ya Burigi, Biharamulo na Kimisi inapatikana katika Wilaya za Biharamulo, Karagwe na Muleba katika Mkoa wa Kagera huku ikiwa umbali wa kilometa 106 kutoka wilayani Chato mkoani Geita.

Amesema umbali huo unaifanya Wilaya ya Chato kukosa sifa ya kuitwa jina la hifadhi hiyo huku akiomba pia geti la kuingilia ndani ya hifadhi hiyo liwekwe katika Wilaya ya Biharamulo ambayo iko karibu na ni umbali wa kilometa 82 kutoka mji wa Biharamulo.

Akiwasilisha hoja za wananchi katika ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan wilayani Biharamulo huku akidai jina hilo limeleta mvutano miongoni mwa wananchi wa wilaya hiyo huku wakiona dalili za kuporwa hifadhi hiyo.


 
“Hifadhi hii tangu imeunganishwa imeleta kelele kwa watu wa Biharamulo. Mzozo umekuwa mkubwa, wakati wa kampeni nilipata shida kweli wananchi wanasema wamedhurumiwa hifadhi yao. Wanajiuliza iweje hifadhi iko Biharamulo lakini inaitwa jina la Chato kilometa 106 kutoka hapa, huwezi kuingia hifadhini kabla hujapita hapa na geti la kuingia hifadhini ni kilometa 82 hapa,” amesema.

“Tunaomba ili kufanya haki kwa watu wa Biharamulo na Kagera jina hili libadilishwe libaki tu Burigi ili kila mtu aone ni kwake kuliko sasa hivi inaleta ukakasi kwa watu hawa wakaona wameonewa, tunaomba geti watu wa Biaharamulo ili kipindi wageni wanakwenda kwenye hifadhi wasizungukie mbali wapite hapa katikati ya mji wetu waingie kwenye hifadhi,” ameongeza Chiwelesa.

Akitolea ufafanuzi suala hilo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema jina hilo halina utata wowote huku akiahidi kushughulikia hoja ya geti la hifadhi hiyo kuhamishwa na kupelekwa Biharamulo.


"Jina mimi ninavyojua inaitwa Burigi kwa hiyo utata wa jina haupo. Kilichobaki ni geti ambalo nalichukua nakwenda kufanyia kazi. Serikali tunaendelea na sera ya kupeleka maendeleo kwa wananchi, tukikusanya nyingi tutazileta nyingi kwa sababu sisi hatuna faida ya kukaa nazo kule na kuziona zinatuna kwenye mifuko," amesema Rais Samia.


 


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad