Mshambuliaji Mpya wa Simba SC Moses Phiri amesema yupo tayari kuisaidia klabu hiyo kuanzia msimu ujao, baada ya kukamilisha mpango wa usajili wake, akitokea nchini kwao Zambia.
Phiri alitambulishwa rasmi kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC jana Jumatano (Juni 15), kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za klabu hiyo, ambayo imepoteza heshima ya mataji msimu huu 2021/22.
Akizungumza katika mahojiani maalum kupitia Simba TV, Mshambuliaji huyo amesema anafahamu lengo kuu la usajili wake ndani ya klabu ya Simba SC ni kurejesha hadhi na heshima ya klabu hiyo, hivyo atapambana kwa kushirikiana na wenzake ili kufikia lengo hilo kuanzia msimu ujao.
“Sikuja hapa ili niwe mmoja wa wachezaji bora Tanzania, nimekuja hapa kusaidia Simba SC kufikia malengo yake, ikiwa tutakuwa na timu nzuri, mawasiliano mazuri na ushirikiano, naimani tunaweza kushinda Ligi ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.”
“Mimi ni mtu ambaye huwa siogopeshwi na Presha za Mashabiki. Muda mwingine huwa najihisi kama huwa nacheza vizuri zaidi ninapocheza kwenye Presha kubwa kwa kuwa ndio kazi yangu niliyoichagua. Kucheza chini ya Presha ni vizuri, hii inategemea na utakavyoweza kuimudu.” Amesema Phiri
Phiri amejiunga Simba SC baada ya kumaliza mkataba wake na Zanaco FC, ambayo msimu uliopita aliitetea kwenye michuano ya Ligi ya Zambia na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.