Mbeya. Mtu mmoja amefariki dunia na wengine kunusurika katika ajali baada ya roli lililobeba shehena za mizigo likielekea mkoani Dar es Salaam kuferi breki na kugonga magari manne na kisha kuwaka moto katika mtelemko wa barabara kuu ya Mbeya-Iringa eneo la Pipe line Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ,Urlich Matei amesema ajali hiyo imetokea leo Jumatatu June 27, 2022 saa 12 asubuhi.
Amesema ajali hiyo ilihusisha roli la mizigo likiwa linaendeshwa na Erick Ndasigwa (39) mkazi wa Dar es Salaam lilifeli breki na kisha kugonga magari manne likiwepo gari ndogo ambayo dereva wake alipoteza maisha akiwa ndani ya gari.
Matei ametaja watu walionusurika katika ajali ani madereva akiwemo aliyesababisha ajali , Erick Ntasigwa, Yunus Amos, Philimon Bartazali na Abdafik Mohammed (29) mkazi wa jijini Mbeya na dereva wa Shirika Water Reed Tanzania
Matei amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mtelemko mkali uliopo kwenye eneo ilipotokea ajali
Matei ameomba Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) kuangalia uwezekano wa kupanua miundombinu ya barabara kwa njia nne kutokana na kutumika katika usafirishaji wa shehena za mizigo kwenda nchi mbalimbali.
Wamesema mara baada ya kufika eneo la tukio walikuta gari ndogo ikiwa imenasa chini ya roli la mizigo huku kukiwa na mwili wa mtu mmoja aliyeteketea kwa moto.