Mshambuliaji wa Wydad Casablanca Simon Msuva
KIUNGO mshambuliaji wa Wydad Casablanca, Mtanzania Simon Msuva amekiri kufuatwa na kufanya mazungumzo na timu kongwe za Simba na Yanga kwa ajili ya kumsajili kuelekea msimu ujao.
Kauli hiyo aliitoa juzi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara uliozikutanisha Yanga na Coastal Union ya mkoani Tanga.
Kiungo huyo hivi sasa yupo nchini akisubiria hatima ya kesi yake inayoendelea Fifa dhidi ya klabu yake hiyo anayoichezea ya Casablanca.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Msuva alisema kuwa hivi karibuni ataweka wazi wapi anakwenda kati ya timu hizo mbili kongwe hapa nchini.
Msuva alisema kuwa anafahamu Watanzania wengi wanasubiria kusikia wapi atasaini mkataba wa kuichezea kati ya Simba na Yanga.
Aliongeza kuwa amefanya mazungumzo na timu hizo kongwe, lakini bado hajaamua wapi anakwenda kucheza na atatangaza mara baada ya kesi yake kufikia hukumu Fifa.
“Ninafahamu kuwa Watanzania wengi wanaopenda soka wanasubiria kusikia wapi ninakwenda katika msimu ujao, kikubwa wanatakiwa kuwa na subira.
“Timu zote kubwa za hapa nchini zimenifuata kwa ajili ya mazungumzo ya kunisajili lakini bado sijafikia muafaka nazo kwa kuwaomba wanipe muda.
“Kati ya timu hizo, basi moja wapo huenda nikajiunga nayo lakini kama vitu vyangu vitakwenda vizuri vile ninavyotaka,” alisema Msuva.
Na Wilbert Molandi