Mungu Tusaidie...Mtafaruku Mpya Kanisa la KKKT



SIKU chache baada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Konde, Geofrey Mwakihaba, pande mbili zinazohasimiana zimeingia kwenye mtafaruku mpya wa kugombea mali za kanisa.

Mtarafuku huo ulijitokeza juzi wakati wa Ibada ya Jumapili Kanisa la KKKT Ruanda, jijini hapa, mahali alipohamishia makao makuu ya Dayosisi ya Konde, aliyekuwa Askofu wa Kanisa hilo, Dk. Edward Mwaikali.

Hali hiyo ilisababisha Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wa kanisa hilo na kuwasweka mahabusu.

Waliokamatwa katika sakata hilo ni aliyekuwa Mkuu wa Jimbo la Mbeya Mashariki, Nyibuko Mwambola na Dk. Mwaikali, ambao walipelekwa mahabusu wanakoendelea kushikiliwa.

Kabla ya kukamatwa kwa viongozi hao, Mchungaji Mwambola akiwa madhabahuni alitoa taarifa kwa waumini wa kanisa hilo kuhusu uamuzi wao wa kujitenga na Kanisa la KKKT na kujiunga na Kanisa la Kilutheri la Afrika Mashariki.


Hata hivyo, muumini mmoja alisimama na kuhoji uhalali wa uamuzi huo, ndipo alipochukuliwa na viongozi hao na kumwingiza kwenye gari na kutaka kuondoka naye kusikojulikana kabla ya mtu huyo kuokolewa na askari wa Jeshi la Polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ulrich Matei, alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na kuwekwa mahabusu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu jana, Kamanda Matei alisema kwa kifupi kuwa wanawashikilia viongozi hao kwa ajili ya mahojiano zaidi.


“Ni kweli tunawashikilia Mchungaji Mwambola na aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Konde, Dk. Mwaikali kwa mahojiano zaidi, kwa sababu tunatambua kuwa mgogoro wa Dayosisi hiyo ulikwisha baada ya kusimikwa kwa askofu mwingine, lakini inaonekana wao bado wanaendelea na mgogoro huo,” alisema Matei.

Wakati hayo yakijiri, uongozi mpya wa Dayosisi ya Konde chini ya uongozi wa Askofu Mwakihaba, unadaiwa kuwatuma mabaunsa pamoja na madalali wa Mahakama, kufunga ofisi zilizokuwa zikitumiwa na uongozi uliopita wa Dk. Mwaikali zilizopo kwenye Kanisa la Usharika wa Ruanda.

Hatua ya kufungwa kwa ofisi hizo, ilisababisha waumini wa kanisa hilo, hasa wanaoaminika kuwa ni wafuasi watiifu wa Dk. Mwaikali, kukusanyika kuzuia uongozi mpya kufanya shughuli zozote ndani ya kanisa hilo kwa madai kuwa wao bado wanamtambua Dk. Mwaikali kuwa ndiye askofu wao.

Mvutano huo wa waumini wa KKKT, ulisababisha Jeshi la Polisi kufika kanisani hapo ili kuwatawanya wafuasi wanaoendelea kumtambua Dk. Mwaikali kuwa ndiye askofu wao, na kupinga hatua iliyofanywa na viongozi wanaodaiwa kuwa wa askofu mpya kufunga kanisa hilo ili kulinda mali zote za kanisa zisitumiwe na askofu aliyevuliwa madaraka.


Mkuu wa Operesheni ya Jeshi la Polisi Mbeya Mjini, Johanes Bitegeko, aliwaamuru waumini waliozingira kanisa hilo kutawanyika mara moja kwa kile alichoeleza kuwa wanafanya mikusanyiko isiyokuwa rasmi.

Aliwataka waumini hao kuwa watulivu wakisubiri maamuzi kutoka mamlaka husika kutoa maelekezo ya kumaliza mgogoro huo ambao umedumu takribani miaka miwili sasa.

“Mgogoro huu bado unashughulikiwa, nawataka waumini kuwa watulivu, sisi kazi yetu ni moja tu kulinda usalama wa raia na mali zao na nyie mmekusanyika hapa bila sababu ya msingi, ondokeni mkaendelee na shughuli nyingine za uzalishaji mali na mambo mengine ya msingi kwa sababu mgogoro huu hautatuliwi chumbani, maamuzi yatakapotolewa kila mtu atajua na huduma zitaendelea, tunaomba muondoke,” aliamuru afande Bitegeko.

Dalali wa Kampuni ya Pamoja Auction Mart, aliyehusika kulifunga kanisa hilo, Lwitiko Mwamaso, alisema uongozi mpya chini ya Askofu Geofrey Mwakihaba, ulimwagiza kwenda kufunga ofisi za kanisa hilo, baada ya aliyekuwa Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk. Mwaikali kutangaza Usharika wa Ruanda kujiunga na Kanisa la Kilutheri la Afrika Mashariki.


Alisema tayari kanisa hilo limejiunga na kanisa jipya na kuamua kubadilisha bango kutoka Kanisa la Kuu la KKKT Dayosisi ya Konde Ruanda na kuweka linalosomeka ‘Kanisa la Kilutheri la Afrika Mashariki’.

Emmanuel Mwaisanga, kutoka Usharika wa Sinai jijini Mbeya, alisema ameshtushwa kuona usharika wa Ruanda umejitenga na kuanzisha kanisa lao na kwamba hawako tayari kuona ushirika huo unajitenga kwa sababu ni watoto wa baba mmoja.

“Hakuna mtu atakayesimama na kusema amejenga usharika huo wa Ruanda bali kila mwana KKKT kote nchini alishiriki aidha kwa sadaka au njia nyingine kujenga, sio sawa waumini hao kuanza kujimilikisha kanisa hilo na kudai ni mali yao na kuanzisha kanisa lao,” alisema Mwaisanga.




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad