Jeshi la Polisi mkoa wa Geita linaendelea na uchunguzi juu ya tukio la Petro Peter 18, mwanafunzi wa shule ya sekondari Biteko, ambae amekutwa amejinyonga mpaka kufa kwa kutumia mkanda wa suruali na tai nyumbani kwao asubuhi ya Juni 4, 2022.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Henry Mwaibambe, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kijana huyo alijinyonga baada ya wazazi wake kwenda kwa mtendaji kutoa taarifa za yeye kurejea nyumbani baada ya kutoweka nyumbani kwao kwa muda kwa wiki mbili.
"Huyu mtoto alijinyonga akiwa nyumbani kwao kwa kutumia mkanda wa suruali na tai ya shuleni, chanzo cha tukio wiki mbili kabla alikuwa ametoroka nyumbani, kwenda kusikojulikana, wazazi wakaripoti kwa Mwalimu Mkuu ambao walishirikiana na Mtendaji kumtafuta na kutoa wito atakaporudi wamjulishe ili amkamate ampeleke shuleni, tarehe 4 asubuhi akawa ameonekana wazazi wakaenda kumjulisha mtendaji walivyorudi wakakuta mtoto tayari ameshajinyonga,"amesema Kamanda Mwaibambe.
Aidha Kamanda Mwaibambe, ametoa rai kwa wazazi nchini kutoa taarifa endapo watoto wataonesha dalili za kuanza kujiunga na makundi yasiyofaa ili kuwaepusha kujiingiza katika vitendo vya kihalifu.