KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi amewarudisha mastaa wake wote ambao hawajaitwa timu za taifa na kuwapeleka gym kujifua kwa muda wa siku nne, ili kujiweka tayari kwa mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union, huku akiishangaa Simba kumtema Pablo Franco.
Nani amesema ameshtuka mno kusikia kocha mwenzake amepigwa chini siku chache baada ya kumalizika kwa pambano lao la nusu fainali ya ASFC iliyopigwa jijini Mwanza na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 akibainisha Simba imepoteza kocha wa kuwapa mafanikio msimu ujao.
Simba imetangaza kumtema Pablo akiwa ameitumikia timu hiyo kwa muda wa siku kama 204 tu baada ya kulitema taji hilo la ASFC iliyokuwa inalishikilia kwa misimu miwili na akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema hata kama Simba ilipoteza mataji yake ya ndani msimu huu, lakini nafasi ya kulaumiwa kocha Pablo haikuwa kubwa kiasi cha kutakiwa kutimuliwa.
“Huo sio uamuzi wa watu wanaoangalia maslahi ya soka na afya ya klabu, nafikiri alipambana sana kufukuzana na sisi kwenye ligi na hata mashindano ya CAF, nimeshtushwa na kusikitishwa na huo uamuzi,” alisema Nabi.
Nabi alisema ingawa Pablo hakuwa na uzoefu mkubwa wa soka la Afrika akiweka alama ya kwanza akiwa na Simba lakini kwa mwanzo wake haukuwa mbnaya na kwamba aliamini msimu ujao angeanza kufanya vizuri zaidi kama angepewa muda.
“Niliona hakuwa kocha ambaye amefanya kazi hapa Afrika lakini ukiona kazi yake ya kwanza unaona kwamba alikuwa kocha mzuri ambaye mawazo yangu niliona alitakiwa kupewa msimu mwingine kuendeleza ubora wake.
“Niliongea naye wakati wa mchezo wa nusu fainali, nilimwambia amekuwa na mwanzo mzuri wa kufanya kazi hapa Afrika na nikamwambia kama uongozi wake utampa ushirikiano angeweza kuleta ushindani zaidi msimu unaokuja lakini bahati mbaya wamemwondoa.
“Maisha yetu makocha yako hivyo, tunapata kazi ambazo wakati wowote unaweza kuipoteza, ninachojifunza hapa Tanzania na hata sehemu zingine ni watu watakupa muda wa kupenda kazi yako ukiwa unafanya vizuri lakini siku ukifanya vibaya jiandae kwa maamuzi magumu.”