KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi ameondoka nchini jana kenda mapumziko nchini Ubelgiji, lakini alipoulizwa kuhusu usajili wa Bernard Morrison Yanga akahamaki na kusema; “Morrison? Namwachaje.”
Ameliambia Mwanaspoti kwamba amekiangalia kikosi cha Simba na rundo la mastaa wake wote wanaopigiwa hesabu za kutemwa na kubaki akisema kuna mmoja au wawili pekee wanaweza kupata namba kwake, Morrison akiwemo ila kwa masharti.
Morrison ni kama ameshaachana na Simba kwani licha ya kudai kwenye barua yao kwamba wamempumzisha kwa muda, lakini wamemtakia kila la heri kwenye maisha yake ya soka na hata yeye inaripotiwa ameshawaaga wenzie na ametoa vitu vyote vinavyohusiana na Simba kwenye akaunti zake.
Nabi alisema Morrison ni winga bora mwenye kipaji cha kushtua ambaye anaweza kufumba macho yake kisha akamsajili bila kujali sana nidhamu yake na akamsaidia.
Kocha huyo alisema kama GSM wataamua kumsajili winga huyo anatamtumia katika kuboresha kikosi chake katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
“Simba kuna watu wawili tu, lakini jina la kwanza ambalo ningelisajili ni Morrison ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu sana, ingawa ana shida zake bado nafikiria kuleta winga mwenye ubora kama wa Morrison,” alisema Nabi.
“Sijui kama viongozi wangu kama wamemsajili lakini kama tutakuwa na mtu kama yule (Morrison) tutakuwa na nguvu kubwa kwa msimu ujao hasa mashindano ya CAF,” alisema kocha huyo bila ya kujali kelele za mashabiki wa Yanga mitandaoni ambao wanadai hawamtaki arudi.
Akizungumzia nidhamu ya Morrison aliyewahi kuishtaki Yanga CAS, alisema suala hilo atawaachia viongozi wake kisha yeye atajihusisha na kipaji chake ndani ya uwanja pekee.
“Ni kweli tunatakiwa kuwa na watu wenye nidhamu kwenye timu. Huu ni msingi mkubwa, lakini wachezaji wazuri wengi ni watukutu. Kama atasajiliwa hapa mimi nitaangalia sana ubora wake uwanjani na uongozi nao uangalie jinsi ya kumfanya atulie acheze mpira.
“Niliambiwa alikuwa hapa kabla nafikiri kama unasikia kama ambavyo mimi nasikia kwamba anaweza kuja, basi watakuwa wanajua ni jinsi gani watamfanya atulie na acheze. Ngoja tusubiri kwa kuwa sasa muda bado kidogo kuliona hilo kwa uhalisia uliokamilika.”
Kocha huyo alisema kuwa katika hesabu zake za msimu ujao anahitaji winga bora zaidi ya alionao kwa sasa katika kikosi ili kumuongezea nguvu ya kusaka mabao.
Inadaiwa Morrison ameshafanya mazungumzo ya kina na viongozi wa Yanga, lakini bado kulikuwa na mvutano mdogo juu ya kumrejesha Jangwani ingawa kama wakimuinulia Nabi simu moja tu staa huyo huenda akaonekana kwenye jukwaa la Jangwani kabla msimu haujamalizika.
L