Joseph Selasini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR Mageuzi
CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimetangaza baadhi ya wajumbe wapya wa Sekretarieti ya chama hicho, baada ya kuvunja iliyokuwa inaongozwa na Mwenyekiti wake, James Mbatia, anayedaiwa kusimamishwa uongozi na Halmashauri Kuu yake, Mei 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Wajumbe hao wametangazwa leo Ijumaa, tarehe 17 Juni 2022 na Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Martha Chiomba, katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Ilala jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa wajumbe hao ni Joseph Selasini, aliyeteuliwa kuwa Katibu wa Idara ya Uenezi. Joseph Magabe (Idara ya Fedha, Uchumi na Mipango), Hassan Said (Idara ya Katiba, Sheria, Haki za Binadamu).
“Selasini atakuwa mwenezi wetu na kijiti kikubwa tunamuachia yeye azunguke kwa sapoti yangu. Tutazunguka naye nchi nzima na sasa tunamaanisha hakitakuwa chama cha mikutano ya wanahabari, hiki ni chama cha wananchi, tutarudi kwa wananchi kwa vitendo,” amesema Chiomba.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Haji Khamis, amesema mkutano mkuu wa chama hicho utaitishwa wakati wowote kuanzia sasa, huku akidai hawana migogoro kwa kuwa imeshatatuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho iliyoketi Dar es Salaam, Mei 21, 2022 na kumsimamisha uongozi aliyekuwa Mbatia na sekretarieti yake.
“Masuala ya vikundi, majungu, mitafaruku iwe basi. Kuanzia sasa chama kimerudi kikiwa kimoja na mkutano mkuu wa taifa utakaoitishwa wakati wowote kutoka sasa utaleta maamuzi ya muafaka ambayo huwa yatategemea kutoka maamuzi ya halmashauri kuu ya taifa,” amesema Khamis.