NCCR wahofia mazungumzo ya Mbatia na Msajili


Q

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku mbili tangu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia kukutana na Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho (Zanzibar), Ambar Khamis amesema wanapata shaka baada ya kuona taarifa hizo.

Mei 30 mwaka huu Jaji Mutungi alikutana na Mbatia, akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa chama hicho, Ofisi ndogo jijini Dar es Salaam ambapo maongezi yao yalikuwa ya siri na yalidumu kwa zaidi ya saa matano.

Mbatia, ambaye alisimamishwa kujihusisha na shughuli za chama, pamoja na Makamu Mwenyekiti wake (Bara) Angelina Mtahiwa kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu uliofanyika Mei 21 na baadaye Ofisi ya Msajili kubariki uamuzi huo, juzi baada ya kukutana na Jaji Mutungi alisema, mazungumzo hayo yalikuwa ni hatua za mwanzo za kuhakikisha Tanzania inakuwa mahali salama pa kuishi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ambar, ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho alisema baada ya kuona taarifa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikiwemo ‘magrupu’ ya chama kuwa Mbatia na wenzake wamesharidhiana walipata mshtuko.


 
“Msajili amuache Mbatia aje kwenye Mkutano Mkuu, ajieleze kwa wajumbe endapo wataridhika wataamua, Msajili yeye asimamie maamuzi yake mwenyewe ambayo alishayatoa,” alisema Ambar.

“Sio tatizo Msajili wa Vyama vya Siasa kukutana na mtu au kiongozi wa chama chochote na kuongelea masuala ya vyama, ila tulipata mshtuko kuona Msajili anakutana na mtu ambaye tulimsimamisha,” alisema.

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema wapo kwenye vikao tangu asubuhi na kutaka apewe muda ili aweze kufuatilia na kutoa ufafanuzi.


“Tangu asubuhi tuko kwenye vikao, lakini hata maswali unayouliza sijasona hiyo taarifa, nashauri unipe muda nifuatilie ili niweze kutoa ufafanuzi,” alisema Nyahoza.

Aidha, Makamu huyo alisema kanuni zinaruhusu kwenda kukutana na Msajili, ila mshtuko uliopo ni kwamba Mbatia alikwenda kwa mantiki gani.

“Msimamo wetu ni kuwa NCCR-Mageuzi hakuna mgogoro wa uongozi unaoweza kupelekea kupatanishwa na Msajili, kilichotokea ni mabadiliko ya uongozi kwa mujibu wa sheria, hivyo jukumu la Msajili ni kuchunguza uhalali wa kikao husika na maamuzi yake.”

Aliongeza kuwa hayo yalikuwa ni mambo yao ya ndani, ya kukisafisha chama na kumuomba Msajili awaache kwa kuwa wameshatekeleza wajibu wao.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad