Babati. Mkazi wa Kijiji cha Vilima Vitatu wilayani Babati mkoani Manyara, Mashaka Boay (41) amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kukutwa na nyama ya twiga.
Hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Babati, Victor Kimario ametoa hukumu hiyo baada ya mahakama hiyo kumtia hatiani Boay.
Hakimu Kimario amesema Boay ametenda kosa hilo Machi 23 mwaka huu kwenye kijiji cha Vilima Vitatu.
Amesema Boay amekutwa na nyama ya twiga ambapo thamani ya mnyama huyo ni Sh34 milioni.
Hata hivyo, Boay aliiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu amesema hilo ni kosa lake la kwanza.
Pia, amesema ana watoto wanne wanaomtegemea hivyo mahakama hiyo impunguzie adhabu.
Hakimu Kimario amesema kosa hilo ni la uhujumu uchumi hivyo Boay anahukumiwa kifungo cha miaka 20 kwenda jela.