ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania,Lengai Ole Sabaya amecharuka mahakamani na kudai mashtaka dhidi yake ni ya uonevu ndiyo maana upande wa mashtaka umeshindwa kukamilisha upelelezi ili kesi hiyo ianze kusikilizwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).
Sabaya na wenzake wanne wanakabiliwa na mashtaka saba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi mkoani Kilimanjaro yakiwemo kuunda genge la uhalifu, rushwa na utakatishaji fedha.
Alitoa shutuma hizo jana Jumatatu tarehe 20 Juni 2022 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Salome Mshasha wakati kesi hiyo ilipokuja kwa kutajwa.
Hatua hiyo ya Sabaya kuja juu ilitokana na mawakili wa upande wa mashtaka kuomba muda zaidi kwa kile walichodai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika wakati 1 Juni 2022 walidai upelelezi umekamilika na kuomba ahirisho fupi kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali ya makosa yao.
Sabaya alidai mahakamni hapo kuwa huko magereza siyo sehemu nzuri na hawaendi pikiniki hivyo upande wa mashtaka kuendelea kudai upepelezi haujakamilika ni kuendelea kuwatesa bure.
“Mheshimiwa naendelea kusisitiza kesi hii ni ya uonevu, leo mimi nafanyiwa hivi na ni mtumishi wa umma je hao ambao siyo watumishi wa umma ni wangapi wanaofanyiwa haya? Ikumbukwe mheshimiwa tulitolewa gerezani usiku katika mazingira ya kutisha,” alisema Sabaya
Alidai wanaomshitaki huku akiitaja Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wanajua mashitaka hayo ni ya kutengeneza ndiyo maana kila mara wanadia upelekezi haujamalika kwa sababu hawana ushahidi ni kile wanachomshitaki nacho.
Kesi hiyo ilikuja tena kwa mara ya tatu ambako wakili wa serikali, Velediana Mleza aliomba ahirisho la siku 14 kwa madia upelelezi haujakamilika hali ambayo iliwalazimu mawakili wa upande wa utetezi kuja juu.
Mawakili hao Hellen Mahuna na Hekima Mwasipu wadai 1 Juni 2022 upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba ahirisho fupi ili kuwasilisha nyaraka za kuipa mamlaka mahakama ya hakimu mkazi kuanza kusikiliza shauri hilo na kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali ya kosa.
Waliutaka upande wa mashitaka kuwa makini na kile wanachowasilisha mahakamani kwani wateja wao wanahitaji kutendewa haki huku pia wakiendelea kusisitiza mshitakiwa wa kwanza, Lengai Ole Sabaya ni mgonjwa.
Lengai Ole Sabaya akiwa mahakamani Arusha
Hakimu Mshasha alikubaliana na hoja za upande wa utetezi na kuutaka upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi huo na kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe 4 Julai 2022 itakapotajwa tena.
Mbali na Sabaya, washtakiwa wengine ni, Silivester Nyegu, John Aweeyo, Nathan Msuya na Antero Assey.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, shitaka la kwanza ni la kuunda genge la uharifu shitaka linalowahusu washitakiwa wote ambako Februari 2021, Sabaya akiwa mtumishi wa umma kama mkuu wa wilaya ya Hai alikiuka majukumu yake ya kiutendaji kwa makusudi na kwa nia ya kutekeleza jinai walijipatia Sh.30 milioni.
Shitaka la pili lilimhusu Sabaya peke yake ambako anadaiwa Februari 2021 wilayani Hai kwa nia ya kutenda kosa alishawishi na kudai rushwa ya Sh.30 milioni kutoka kwa Godbless Swai na tarehe hiyo hiyo alijipatisa Sh.30 milioni kama rushwa kutoka kwa Elibariki Swai kwa nia ya kuzuia taaarifa za kiuchunguzi kuhusiana na ukwepaji wa kodi.
Shitaka la tatu na la nne liliwahusu washitakiwa wanne, Silvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey ambao wanadiawa kwa pamoja kuwa mnamo Februari 2021 huko wilaya ya Hai walisaidia kutendeka kwa jina.
Wanadaiwa katika tarehe hiyo washitakiwa hao walimsaidia Sabaya kuweza kushawishi na kumsaidia kupata Sh.30 milioni kutoka kwa Alex Swai huku pia wakidaiwa kumsaidia Sabaya kujipatia manufaa asiyostahili kwa kujipatia Sh.30 miliuoni kutoka kwa Alex Swai.
Sabaya pia anadaiwa katika shitaka la sita linalomhusu yeye mwenyewe kuwa alitenda kinyume na na mamlaka yake kwa kutumia nafasi yake kama mkuu wa wilaya kwamba alinajisi nafasi yake ya mkuu wa wilaya kwa kuanzisha mashitaka dhidi ya Alex Swai kuwa amekwepa kodi na kujipatia Sh.30 milioni kwa manufaa yake na wenzake wanne.
Shitaka la saba ni la utakatishaji wa fedha linalowahusu washitakiwa wote ambako Februari 2021 huko wilaya ya Hai kwa pamoja na kwa nia moja walijipatia Sh.30 milioni huku wakijua fedha hizo ni zao la uharifu.
Baada ya kusomewa mashitaka yao, washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza mashauri ya uhujumu Uuchumi hadi kupata kibali cha mahakama kuu.