STRAIKA mpya wa Simba, Mzambia Moses Phiri amewaambia mashabiki kwamba lengo lake la kwanza ni kubeba makombe.
Phiri ambaye amesaini miaka miwili Simba alisema ameridhia kujiunga na klabu hiyo kutokana mpangilio mzuri aliouona kuanzia kwenye uongozi mpaka jinsi wachezaji wanavyoishi na hata Wazambia wenzie, Clatous Chama na Larry Bwalya wamemwambia Simba ni sehemu freshi zaidi.
“Kitu cha muhimu sana ni kushinda vikombe na kuisaidia timu. Nikipata ushirikiano mzuri nitafanya kazi kubwa,naahidi tutarudi kwenye kasi yetu ya kushinda vikombe”. alisema Phiri na kuongeza
“Siwezi kuahidi kwamba nitafunga kila mechi lakini kwa uwezo ambao ninao nitafanya kile ambacho mashabiki wanakitaka, nimezoea presha na hii ndio kazi niliyochagua,siko hapa kuwa staa wa nchi nimekuja kuisaidia klabu”.
“Mashabiki wanapaswa kuwa wavumilivu siyo kuanza kukosoa tu, ninaamini kwa ushirikiano wa wenzangu Simba inaweza hata kushinda ubingwa wa Afrika,” alisema huku Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Seleman Matola akisema wamemsainisha kimkakati.
Aidha Matola alisema, Phiri ni mtu sahihi; “Kaja kwa wakati sahihi, tunasajili mchezaji kutokana na mahitaji naamini atafanya vizuri kwa kushirikiana na wenzake ndani ya kikosi,”alisema Matola ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba na Supersports ya Afrika Kusini.
Mshambuliaji wa sasa Simba Chris Mugalu alisema; “Nyie wenyewe mtamuona ni mchezaji mzuri sana atasaidia timu yetu kama Mungu akijaalia nikiwepo msimu ujao basi tutafanya kazi nzuri sana na watatupenda, nisipokuwepo naamini atashirikiana vyema na watakaokuwepo.”
Mugalu alisema Phiri ni mchezaji anayeweza kufunga kutoa pasi na uwezo wa kutumia vyema eneo lake la kufunga hivyo wapenzi wa Simba watafurahi kuona kiwango chake kwani ni moja ya wachezaji wenye uwezo wa kuwasumbua mabeki wa timu pinzani muda wote anapokuwa uwanjani kutokana na aina yake ya uchezaji.
“Faida nyingine kwake anaweza kupiga mipira iliyokufa kwa maana hiyo kama atakuwa bora katika kiwango hicho nilichomuacha nacho mara ya mwisho ni moja ya usajili mzuri huu.”
Huku Larry Bwalya alisema anamfahamu vyema Phiri kwa kuwa wanakutana katika michezo mbalimbali ya timu za Taifa anaujua uwezo na ukubwa wake katika kuisaidia timu kupata matokeo.
“Ni mchezaji mzuri sana, naamini atakisaidia kikosi kuelekea msimu ujao na michuano ya Kimataifa,”alisema Bwalya moja ya wachezaji wanaotarajiwa kutokuwepo msimu ujao baada ya timu ya Amazuru ya Afrika Kusini kuonyesha nia ya kumuhitaji.
Bwalya alisema; “Ni mzambia mwenzangu na uwezo anao mkubwa tu kwa usajili wake ni bora kwa timu hasa katika eneo lake la ushambuliaji.”