MBUNGE Viti Maalum, Esther Matiko, amedai Kituo cha Polisi cha Kigonga, kilichopo wilayani Tarime, katika mpaka wa Tanzania na Kenya, kimekimbiwa na polisi wake kwa kuwa kimejengwa kwa mabati. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Matiko ametoa kauli hiyo leo Jumanne, tarehe 14 Juni 2022, bungeni jijini Dodoma, ambapo amehoji lini Serikali itajenga kituo hicho.
“Kituo cha Polisi cha Kigonga kinawahudumiwa wananchi wa mpakani mwa Tanzania na Kenya katika kata nne, lakini kilijengwa kwa full suti ya mabati kana kwamba kimechakaa na polisi wamekimbia hawapo pale. Nilitaka kujua lini Serikali itajenga kituo hiki sababu ni cha mkakati na ukizingatia kipo mpakani?” aalihoji Matiko.
Akijibu swali hilo la nyongeza, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini, amesema hakuna kituo cha polisi kinachojengwa kwa mabati na kama kipo hakistahili kufanya kazi.
“Viwango vyetu vya kujenga vituo vya Polisi sio kuwa full suti ya mabati. Kwa hiyo kama kuna kituo cha aina hiyo hakikidhi viwango.
“Pengine niwasiliane na mbunge na mamlaka za serikali za mitaa ili tuanze kujenga kituo kwa kutumia vifaa vya kudumu ikiwemo matofali na kadhalika,” amesema Sagini.