R. Kelly ahukumiwa miaka 30 jela katika kesi ya unyanyasaji wa kingono




Mwimbaji wa Marekani R. Kelly amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kutumia hadhi yake kuendesha mpango wa kuwadhalilisha kingono watoto na wanawake.

Mnamo Septemba, mahakama ya New York ilimtia hatiani msanii huyo wa R&B,   mwenye umri wa miaka 55, kwa makosa ya ulanguzi na biashara ya ngono.


 
Mzaliwa huyo wa Chicago - ambaye jina lake halisi ni Robert Sylvester Kelly - pia alipigwa faini ya $ 100,000 (£ 82,525).

Kwa sasa anakabiliwa na mashtaka tofauti ya uhalifu katika kesi nyingine tatu.

Kelly - anayejulikana kwa nyimbo maarufu kama I Believe I Can Fly na Ignition - alipatikana kuwa alitumia hali yake ya umaarufu na nyanja ya ushawishi kuwavutia wanawake na watoto katika unyanyasaji wa kijinsia kwa zaidi ya miongo miwili.



Katika hukumu yake siku ya Jumatano, Jaji wa  korti ya Wilaya ya Marekani Ann Donnelly alisema mtu mashuhuri alitumia ngono kama silaha, na kuwalazimisha waathiriwa wake kufanya mambo yasiyoweza kuelezeka na kuwaambukiza  na magonjwa yasiyotibika.

Adhabu hiyo, alisema, itakuwa  kama kizuizi dhidi ya kufanya uhalifu kama huo katika siku zijazo.

Majaji katika kesi ya Kelly ya wiki sita huko Brooklyn walisikia jinsi alivyosafirisha wanawake kati ya majimbo tofauti ya Marekani , akisaidiwa na mameneja, walinzi na wanachama wengine wa msafara wake .

Mahakama pia ilisikiliza jinsi Kelly alipata hati za ndoa na mwimbaji Aaliyah kinyume cha sheria alipokuwa na umri wa miaka 15 mwaka wa 1994, miaka saba kabla ya mwimbaji huyo kufariki katika ajali ya ndege.


 
Cheti hicho, kilichovuja wakati huo, kiliorodhesha umri wa Aaliyah kuwa 18. Ndoa hiyo ilibatilishwa miezi kadhaa baadaye.

Waendesha mashtaka wa serikali walikuwa wamependekeza kwamba Kelly ahukumiwe kifungo cha zaidi ya miaka 25, kutokana na uzito wa uhalifu wake na "haja ya kulinda umma dhidi ya uhalifu zaidi".

Lakini mawakili wake walitaka kifungo cha miaka 10 - kiwango cha chini cha lazima kwa kuhukumiwa kwake - au chini ya hapo.

Walionyesha Kelly kama aliyekua katika hali ya  umaskini katika maisha  yaliyojaa unyanyasaji wa nyumbani na kuteswa kuanzia akiwa na  umri mdogo. 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad