Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametaja sababu za kukubali kushiriki kwenye tamasha la msanii wa muziki wa HipHop, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu ‘The Dream Concert’ huku akizindua kitabu cha muziki na maisha cha mwanamuziki huyo.
Tamasha hilo limefanyika usiku wa kuamkia leo Jumatano Juni Mosi kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam likiwa ni maalumu kwa mbunge huyo wa zamani wa Mbeya Mjini kuadhimisha miaka 30 kwenye sekta ya muziki.
Akieleza sababu ya kukubali kushiriki tamasha hilo, mkuu huyo wa nchi ameweka wazi sababu mbili akisema "Kwanza kwa Joseph mimi ni mama hivyo niliona fahari kushuhudia mafanikio ya mwana”
Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na msanii wa muziki wa Hiphop, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ mara baada ya kuwasili Serena kwa ajili ya kuhudhuria tamasha la maadhimisho ya miaka 30 ya msanii huyo. Picha na Ikulu
Akitaja sababu ya pili, Rais Samia amesema "Lakini pia nilivutiwa na wazo la kuandika kitabu, nikasema naenda kumsapoti, japo tarehe aliyoipanga mwanzo nilikuwa bize, akasema atasogeza mbele na leo niko hapa na nitazindua kitabu chake," amebainisha
Akitaja majina ya utani ya mwanamuziki huyo likiwamo la Taita na Sugu ambalo alisema hawezi kumuita kwa kuwa sasa mwanamuziki huyo huku akikumbusha moja ya tukio la Sugu lililotokea bungeni wakati mkali huyo wa HipHop akiwa anawawakilisha wananchi wa Jimbo la Mbeya Mjini.
"Mimi nitamuita Joseph, nakumbuka siku alipomuudhi Spika akasema mtoeni nje, alishikwa mguu na mkono," amesema Rais Samia.
Amesema safari ya Sugu kwenye tasnia muziki haikuwa rahisi, aliingia wakati bado muziki ukiwa haukubariki.
Katika tamasha hilo, Rais Samia aliweka wazi kuwa kuna kipendi hata yeye alikuwa mtazamo kuwa mziki wa HipHop ni uhuni huku akieleza kuwa mtazamo huo umebadilika.
"Hata mimi nilipokuwa nikiwaona wanafoka foka niliona uhuni wakati ule, lakini kumbe sio kweli, muziki umeleta heshima," amesema.
Rais Samia Suluhu Hassan akiwasili katika ukumbi wa Serena pamoja na msanii wa muziki wa Hiphop nchini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa ajili ya kuhudhuria Tamasha la Dream Concert lililofanyika Serena jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu
Amesema muziki wa Hip Hop hauna maneno ambayo huwezi kusikiliza ukiwa na watoto.
"Hapa wasanii wameimba sijasikia maneno ya kukera, nimeona wabunge na wakuu wa wilaya wakiimba, nikajiuliza wanafanya kazi saa ngapi, lakini wanajua wanavyojigawa, simvunji moyo, nimebariki aendelee tu," amesema.
Rais Samia alizindua kitabu cha msanii huyo chenye jina la Muziki na Maisha from the Street katika tamasha hilo.
Mbowe, Kinana meza moja
Katika tamasha hilo la The Dream Concert Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mpainduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ni miongoni mwa wageni mashuhuri waliojitokeza kwenye tamasha hilo.
Viongozi hao wa ngazi za juu, Mbowe akitoka chama cha upinzani na Kinana akitoka chama tawala wamekaa meza moja na makamu mwenyekiti wa chama tawala.
Hata hiyo, wakati wa hafla hiyo Rais Samia alimuita Mbowe na Kinana wakati wa kuzindua kitabu cha Maisha na Muziki cha Sugu.
Wengine waliopanda jukwaani na Rais Samia ni Waziri wa Utamaduni, Sanaana Michezo, Mohammed Mchengerwana mke wa Sugu.
Mbali na Mbowe na Kinana, wageni waalikwa wengine mashuhuri ni waliohudhuria tamasha hilo ni pamoja na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nauye, Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Msigwa na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika huku wasanii na viongozi mbalimbali wakijitokeza kwa wingi kuungana na Sugu kuadhimisha miaka 30 ya muziki wake.