RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwalea vizuri watoto wao kwani wasipolelewa ipasavyo watazalisha ‘panya road’ wengi, ambao wanaisumbua Serikali na jamii kwa ujumla. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Pia ili kuongeza ufaulu, ametoa wito kwa walimu, wazazi washirikiane kufuatilia maendeleo ya mtoto.
Rais Samia ametoa wito huo leo tarehe 19 Juni, 2022 Visiwani Zanzibar wakati akizindua Taasisi ya masuala ya elimu inayofahamika kwa jina la Mwanamke Initiatives Foundation (MIF).
Rais Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria uzinduzi rasmi wa Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) katika hafla iliyofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar tarehe 19 Juni, 2022. Katikati ni Mwenyekiti na muasisi wa Taasisi hiyo ya MIF, Wanu Hafidh Ameir na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MIF, Fatma Mwasa.
Amesema ni vema wazazi kuwasomesha watoto wa kike na wa kiume kwani wakisomesha wakike peke yake wa kiume akikaa nyuma ni tatizo.
“Tuwasomeshe wote ili waende sambamba, vinginevyo tunaweza tukatengeneza tatizo.
“Ulezi wa kulea mwana sio wa mzazi peke yake, ni mzazi, taasisi, serikali na jamii, wote tulee watoto wetu kwa sababu tusipowalea vizuri tunazalisha panya road, na mnajua wanavyosumbua, kwa wale ambao hamjawaona mnasikia kwenye taarifa za habari,” amesema.
Aidha, ametoa mitihani minne kwa wizara ya elimu, sayansi na teknolojia kwamba iboreshe eneo la mitaala ya elimu nchini.
Amesema kuna wakati mitaala inapishana kati ya Tanzania Bara na Zanzibar hali inayoleta ugumu wa mitihani kwa upande mwingine.
Pili, ameitaka wizara hiyo iboreshe eneo la ukaguzi na utendaji wa wakaguzi hao kiujumla.
“Naomba muangalie suala la wakaguzi wa elimu, utendaji wao, sifa zao lakini pia kuwawezesha vitendea kazi ili waweze kuzunguka kote na kufanya kazi inavyotakiwa, wasiwe tu wakaguzi majina lakini wawe wakaguzi kwa sifa,” amesema.
Tatu ni suala la mitihani yenyewe ambapo ameitaka kufuatilia kwa kina namna utungaji wa mitihani hiyo ya kitaifa unavyofanyika.
Nne, ni sifa za walimu ambapo amesema mwalimu anatakiwa awe amefaulu zaidi katika masomo yake, kabla ya kusomea fani hiyo.
“Sio yule ambaye hajafaulu vizuri kisha amekosa pa kukimbilia, nafasi ya mwisho ndio anaona sasa niwe mwalimu. Hapa ndipo tulipata changamoto kwenye elimu yetu.
“Kama tutatakiwa kuongeza nguvu ili walimu wapate mafunzo ya mara kwa mara, tutafanya hivyo kwa ajili ya walimu,” amesema Rais Samia.
Aidha, amesema alimtahadharisha mwanaye ambaye ndiye muasisi wa Taasisi hiyo ya MIF, Wanu Hafidh Ameir kwamba aanze kufanya kazi kya kuinua sekta ya elimu katika mkoa wa Kusini Unguja kwa sababu ndio mkoa unaoshika nafasi ya mwisho katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.
“Nilimwambia Kusini Unguja performance imeshuka sana, Wanu anza kwenu… likibumbulika unalo la kuwaambiwa,” amesema Rais Samia alivyokuwa akimtahadhrisha mwanaye huyo ambaye pia ni Mbunge wa Viti maalumu CCM.
Amesema baada ya miaka mitatu tangu kuanza kwa taasisi hiyo, sasa matokeo ya mkoa huo yameanza kutia moyo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MIF, Fatma Mwasa.
Amesema ilikuwa ni aibu kwa mkoa anaotoka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushika nafasi ya mwisho kitaifa.
“Mitihani inapomalizika, Waziri wa Elimu ananiletea ripoti za matokeo, cha kwanza nachoangalia ni mkoa wa Kusini Unguja, nikiangalia nashika kichwa. Ni aibu mkoa anaotoka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unakuwa wa mwisho katika ufaulu wa mitihani,” amesema.
Amesema ili kuongeza ushindani kwa walimu na ufaulu, walimu watakaoajiriwa na MIF na wengine wanaojitolea katika taasisi hiyo, wasipewe mikataba ya kudumu ili wajitume.
“Mkiwapa ajira ya maisha, hana haja ya kujihangaisha, mkiwawekea vipindi katika mikataba yao watajipima, ambao hawafanyi vizuri wakatoka hapo ufaulu utaonekana pia, muwe na vipimo vya ufanisi. Ila kama ilivyo sasa hapana!
Awali akitoa taarifa kuhusu taasisi hiyo, Mwassa amesema taasisi hiyo inajenga kituo ambacho kitachukua watoto kuanzia umri wa miaka 10 hadi 25 kisha kuwapatia mafunzo ya ufundi stadi.
Amesema lengo la taasisi na kituo hicho ni kumuinua mtoto wa kike, kuwawezesha kiuchumi vijana wote, kuongeza uelewa kwa jamii katika masuala ya afya ya akili na kutoa uelewa kuhusu masuala ya afya ya uzazi kwa vijana na afya ya mama na mtoto.
Amesema kituo hicho ambacho kitajengwa kwa ufadhuli wa Umoja wa Falme za Kiarabu kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 15, kitakuwa kinatoa wahitimu 1000 kila mwaka.