Rais Tshisekedi asema Rwanda inaendesha "vita ya kiuchumi"




Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Felix Tshisekedi ameituhumu Rwanda kuendesha vita ya kiuchumi na kujaribu kuinyakua ardhi ya Congo ili kujipatia rasimali kubwa ya madini.

Shirika la Habari la Associated Press limenukuu rais Tshisekedi  akisema hali ya usalama mashariki mwa Congo inaendelea kuzorota kwa sababu Rwanda inajaribu kudhibiti sehemu ya ardhi ya Congo yenye utajiri wa madini ya dhahabu na kobalti kwa manufaa yake.

Tshisekedi amesema kinachoendelea ni vita ya kiuchumi ya kuwania rasimali na Rwanda inayatumia magenge yake ya kigaidi.

Hapajawa na majibu yoyote kutoka nchini Rwanda kuhusiana na matamshi hayo ya Tshisekedi, ingawa Rwanda mara kadhaa imekanusha madai ya kuwaunga mkono waasi wa M23 ambao waliukamata mji muhimu mashiriki mwa Congo mapema wiki hii.


 
Kwenye matamshi yake rais Tshisekedi  amewataka viongozi wa kimataifa ikiwemo waziri mkuu wa Uingereza kuikosoa Rwanda bila kificho pindi watakapohudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola baadae wiki ijayo mjini Kigali. "Raia wa mashariki mwa DRC hawana hatia lakini wanashambuliwa na jirani yetu" amesema Tshisekedi.

Matamshi ya kiongozi huyo huenda yatachochea moto kwenye mzozo unaotanuka baina ya mataifa hayo jirani ya eneo la maziwa makuu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad