IMEISHA hiyo! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Yanga kumsainisha mkataba wa miaka miwili, kiungo mshambuliaji wa Simba, Mghana Bernard Morrison, huku ikitaja rasmi tarehe ya kumtangaza.
Morrison ni kati ya wachezaji watakaotua kuichezea Yanga katika msimu ujao wakati kocha mkuu, Mtunisia, Nasrredine Nabi akiendelea kusuka kikosi cha kimataifa akilenga kufanya kweli katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Morrison ni mzoefu wa michuano hiyo akiwa ameichezea Simba mara mbili hadi hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga tayari imemalizana kimyakimya na baadhi ya wachezaji wa kimataifa akiwemo Mzambia, Lazarus Kambole, Mburkinabe Stephane Aziz Ki, beki Mcongo, Joyce Lomalisa Mutambala kutoka Interclube ya Angola na straika Muangola, Adriano Belmiro Duarte Nicolau ‘Yano’ anayeichezea Petro de Luanda ya nyumbani kwao.
Mmoja wa mabosi wa Simba, ameliambia Championi Ijumaa kuwa wamejiridhisha Yanga wamemalizana na Mghana huyo kwa kumpa mkataba wa miaka miwili ya kuichezea timu hiyo.
Bosi huyo alisema kuwa wamepata taarifa za Yanga kumsajili kwa mkataba wa miaka miwili wenye thamani zaidi ya Sh 180 ambayo ni zaidi ya aliyowekewa Simba kabla ya kukataa kusaini na kuchukua maamuzi ya kurejea Yanga.
Bernard Morrison akiwa na uzi wa Yanga
Naye kigogo mmoja wa Yanga, alithibitisha taarifa hizo na kusema kiungo huyo amepangwa kutangazwa rasmi Yanga Juni 29, mwaka huu sita usiku mara baada ya mkataba wake Simba kumalizika.