Kiongozi Mkuu wa madhehebu ya Kiislamu ya Mabohora (Dawoodi Bohoras), Sheikh Syedna Mufaddal Saifuddin ametua Tanzania, kwa ajili ya kufanya ziara ya kiimani na mapumziko mafupi.
Saydna Mufaddal atakuwa nchini kwa takribani wiki mbili ambapo, pamoja na shughuli za kiimani amekuja kuunga mkono azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza na kuifungua nchi hasa kupitia filamu ya Royal Tour.
“Hapa nchini amekuja kuunga mkono malengo ya Royal Tour na yeye mwenyewe na wafuasi wake watakwenda mapumziko na msafara wake wote katika maeneo mbalimbali, na pia iwapo taratibu zitakamilika na akaridhia anaweza kufanya mhadhara wake mkubwa wa kidini Julai hapa nchini, ambapo wafuasi wake kati ya 30,000 hadi 40,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani humfuata na tunajipanga ikitokea hivyo tutawaonesha watu hao na mabohora wengine duniani filamu ya Royal Tour,” alisema mmoja wa viongozi wa dhehebu hilo nchini Zainuldeen Adamjee.
Akimpokea Kiongozi huyo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema amewasilisha kwa kiongozi huyo salaam za Rais Samia ikiwemo utayari wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mhadhara mkubwa wa mwaka wa kiongozi huyo utakaoleta maelfu ya watu hapa nchini.