Sakata la Watu Kuuza Vidole vya Miguu Laifikia Serikali ya Zimbabwe na Wametoa Tamko Hili

 


Serikali ya Zimbabwe imepuuza madai yanayoenea kwamba raia wake wamekuwa wakiuza baadhi ya vidole vyao vya miguu ili kupata mamilioni ya pesa.


Naibu Waziri wa Habari Kindness Paradza ameyataja madai hayo kuwa ni bandia na kuwashauri watu kuyapuuza.


“Tulifanya utafiti juu ya suala hili na tukagundua ni uwongo. Hizi ni taarifa za mitandao ya kijamii zinazolenga kuchafua jina la nchi,” alisema Paradza.


Mbunge huyo aliongeza kuwa amejipa jukumu la kuzuru Ximex Mall na kuwahoji wafanyabiashara waliokanusha madai hayo na kuongeza kuwa kumekuwa na wimbi la watu wanaotembelea maduka hayo tangu hadithi hiyo iliposambazwa, baadhi yao wakitoka vijijini umbali wa kilomita 80.


Kwa mujibu wa gazeti la The Herald la nchini humo, mtu anayedai kuhusika na biashara hiyo amefafanua kuwa alitoa matamshi hayo alipokuwa amelewa.


Habari hizo zilienea kwenye mitandao ya kijamii baada ya watu kadhaa kusambaza picha zao wakiwa kwenye magari ya kifahari wakidai kuwa wameyanunua magari hayo kutokana na kuuza vidole vya miguu.


Katika moja ya video hizo, mwanamume mwenye umri wa makamo alionekana akiwa ameweka mkono kwenye gari mpya aina ya Range Rover huku mwanamume mwingine akiwa tayari kumkata vidole vidogo vya miguu.


Madai hayo yalichochewa zaidi na blogu iliyosema kuwa mnunuzi huyo alikuwa katika eneo la Ximex Mall katika mji mkuu wa Zimbabwe wa Harare.


Alipoulizwa kwa nini yeyote aliyekuwa akinunua vidole hivyo alivihitaji, ripoti hiyo ilionyesha kuwa vilitumika kwa matambiko nchini Afrika Kusini.


Kulingana na taarifa za watu waliohusika na madai hayo, kidole gumba cha mguu kina thamani ya $40,000 (KSh 4.7 milioni), kidole cha kati ni $25,000 (KSh 2.9 milioni) huku kidole kidogo kikipata $10,000 (KSh 1.2 milioni).

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad