Serikali Kuwekeza Katika Lishe Kukabili Utapiamlo



Serikali imeahidi kufanya Uwekezaji Kitaifa katika lishe nchini kama sehemu ya mapambano dhidi ya utapiamlo kuanzia ngazi ya Kaya hadi Taifa kuhakikisha jamii inakuwa salama na kushiriki katika shughuhuli za uzalishaji.


Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu wakati wa kikao kazi  kilichohusisha  Watendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) pamoja na wadau wa maendeleo  kuhusu Masuala ya Lishe nchini katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Juni 08, 2022 Bungeni Jijini Dodoma.


Mhe. Simbachawene alisema kama Taifa ni muhimu kuweka jitihada za pamoja katika mapambano hayo kwani ukosefu wa lishe umekuwa na madhara makubwa kwa watanzania  hivyo kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji kwa ufanisi.


“Uwekezaji kama Taifa katika lishe ni muhimu sana  maeneo  ya msingi ni elimu ya lishe ipo mikoa mingi inazalisha chakula kwa kiwango kikubwa kama Iringa na Mbeya lakini kuna shida kubwa ya utapiamlo hasa kwa watoto  na changamoto hiyo insababisha hasara kwa jamii na Serikali,” alisema Mhe. Simbachawene.


Pia aliongeza kwamba ipo haja ya elimu ya lishe kufundishwa katika shule za msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba ili kuwandaa vijana kuwa mabalozi  wazuri wa lishe katika maeneo  yao au hata watakapofikia hatua ya kujitegemea.


“Unapokosa lishe nzuri unapata matatizo ya afya, kina mama wajawazito kukosa mtoto  afya na  mama mwenye afya nzuri  watoto kuwa na udumavu wa akili na mwili na Serikali itapata hasara kwa sababu ya kuwa na watu wasiyo na afya bora kutokana na maradhi kwa kukosa lishe bora,” aliongeza.


Aidha alisisitiza ushirikishwaji wa viongozi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji, wakuu wa wilaya na Mikoa  kwa kuwapatia elimu ya lishe itakayowasaidia kuwafikia wananchi  katika maneo yao ili kuwa na matokeo chanya  na kufikia malengo yaliyokusudiwa.


“Viongozi hawa wakipatiwa elimu ya lishe bora nini mtu ale, vyakula gani vya muhimu maana watu wanaweza kufikiri kula chakula bora lazima uwe na uwezo la hasha! chakula kwa uwezo wowote unaweza kupangilia kikawa na tija  katika mwili  wako je, uelewa huu upo mpaka  ngazi za chini ? Je, nani afuatilie kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora lazima tutumie ngazi hizi za utawala kujenga Taifa letu,” alisisitiza Mhe. Simbachawene.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) alieleza kwamba kama wataendelea kushirikiana na serikali, kushauri, kuongoza na kumasisha lishe kuhakikisha malengo ya Nchi yanafikiwa ambayo ni kufikia  maendeleo endelevu.


“Hatuwezi kufikia malengo kama hakuna ujumuishwaji wa lishe katika sera, mipango, kuimarsha uratibu na kuhamasisha masuala ya lishe na miradi mbalimbali ya lishe kuifikia jamii kwa wingi zaidi,” alibainisha Mkurugenzi huyo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad