Shirika la Reli Tanzania (TRC) limevunja mkataba na kampuni ya Eurowagon ya nchini Uturuki baada ya kampuni hiyo kushindwa kukamilisha ujenzi wa vichwa viwili vya treni ya umeme na mabehewa 30 ya abiria.
Mkuu wa kitengo cha uhusiano TRC Jamila Mbarouk amesema kwa mujibu wa mkataba huo,
vifaa hivyo vilitakiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka 2021 lakini kwa kuwa Eurowagon ilishindwa kutimiza matakwa ya mkataba na kipande cha kwanza Dar es Salaam mpaka Morogoro kikiwa hatua ya mwisho ya ujenzi, TRC ilisitisha mkataba huo Februari 25 mwaka huu.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu hatua mbalimbali zinazoendelea katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), Jamila
amesema baada ya kuvunja mkataba huo, TRC iliendelea na jukumu la kumalizia ukarabati bila gharama na vifaa vinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.
Amesisitiza kuwa TRC haina mgogoro wa kimapato na kampuni ya Eurowagon kwani ilitimiza matakwa ya kimkataba ya kulipa asilimia 35 na kwa kutimiza masharti ya umiliki wa vichwa vya treni vya umeme viwili na behewa 30 vilishahamia kwa TRC.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Miundombinu ya Reli kutoka TRC, Machibya Masanja amesema mkwamo uliopo sasa katika uchelewaji wa mabehewa ya abiria pamoja na vichwa vya treni vipya umetokana na athari za UVIKO 19.
TRC lilisaini mikataba ya manunuzi ya behewa mpya 1,430 ya mizigo kutoka kampuni ya CRRC ya nchini China, behewa mpya za abiria 59 kutoka kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology Limited ya Korea Kusini, seti 10 mpya za treni za kisasa zenye behewa 80 na vichwa vipya 17 vya umeme kutoka kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini vyenye thamani ya shilingi trilioni 1.18.