Shehena ya Dawa Zakamatwa Dar, Zipo za Kuongeza Nguvu za Kiume



Dar es Salaam. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekamata vifaa tiba na dawa zenye thamani ya Sh294,486,590 milioni ambazo hazijasajiliwa zilizohifadhiwa kwenye ghala bubu lililopo eneo la Mtaa wa Kitumbini katika Kata ya Mchafukoge katikakati ya Jiji la Dar es Salaam.

Miongoni mwa dawa zilizokamatwa katika shehena hiyo ni pamoja na zile za kuongeza nguvu za kiume, zinazotoa mimba, kutibu shinikizo la damu na nyinginezo.

Shehena hiyo imekamatwa leo Juni 28, 2022 kufuatia ukaguzi maalum unaoendelea kufanyika katika Kanda ya Mashariki.

Meneja wa Kanda wa TMDA, Adonis Bitegeko amesema timu imefanya ukaguzi maalum katika ghala bubu kufuatia taarifa za kiinteligensia zilizofuatiliwa kwa muda mrefu.


“Katika ukaguzi tuliofanya tumebaini ghala hili linalomilikiwa na Mtanzania mwenye asili ya India, Ramaiya Rijendra, limehifadhi dawa mbalimbali za binadamu ambazo hazijasajiliwa kwa hiyo ubora, usalama na ufanisi wake haujulikani,” amesema.

Bitegeko amesema baada ya kukamata shehena hiyo, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuziondoa dawa hizo baada ya kuziorodhesha.

Ameongeza kuwa, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kuwatoza faini isiyopungua Sh85 milioni na kuziteketeza kwa gharama zao.

“Tunatoa wito kwa wanaoendelea kufanya biashara hizo haramu kuacha mara moja laa sivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria. Tunawaonya pia wataalamu wa dawa wanaojihusisha na biashara hizi haramu hatutosita kuwafutia leseni zao za kitaaluma, hatutomuacha mtu,” amesema na kuongeza;

Zoezi hilo lilianza jana jioni na kufanyika usiku kucha hadi lilipokamilika asubuhi ya leo Juni 28.

Mtuhumiwa aliyekutwa na shehena hiyo alipohojiwa alikiri kuendesha ghala hilo bubu pasipo na kibali na kinyume na sheria kwa kile alichodai hakufahamu taratibu zinazohusika kusajili na kuendesha biashara hiyo.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. NASHANGAA MADAWA YENYE THAMANI KUBWA HIVYO HALAFU FAINI NDOGO KIASI HICHO!!!!???

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad