Dodoma. Ili kuzitumia fedha za wateja wasiozitumi akaunti zao za benki au simu za mkononi kwa muda mrefu kutokana na sababu tofauti, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali itakamilisha kuandaa mapendekezo ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali Fedha Zilizotelekezwa mwaka ujao wa fedha.
Kwa utaratibu uliopo, mteja ambaye hajaitumia akaunti yake ya benki kwa zaidi ya miaka 12 au yule wa simu ya mkononi kwa muda mrefu, akiba iliyomo hupelekwa Bodi ya Bima ya Amana (DIB) iliyo chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akaunti hizo ambazo huwa hazitumiki kutokana na wamiliki kufariki kwa ajali, kifungo cha gerezani, ugonjwa mahtuti hata safari za nje ya nchi au sababu nyingine bila warithi wao kujitokeza kuzifuatilia.
Akichangia bajeti ya Serikal wiki iliyopita, Mbunge wa Makete, Festo Sanga alihoji fedha zinazoachwa kwenye miamala ya simu na bima pindi mtu anapofariki ni nani anafaidika nazo. Mbunge huyo alisema kuna kiasi kikubwa cha fedha kinapotea na kuzinufaisha kampuni husika kutokana na wananchi wengi kutofuatilia akiba hizo.
Akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2022 bungeni leo, Dk Mwigulu amesema Serikali imelifanyia kazi suala hilo na inakamilisha mapendekezo yatakayowawezesha kutunga Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Fedha Zilizotelekezwa.
“Lengo ni kuweka utaratibu wa kisheria wa usimamizi wa rasilimali kama hizo, Serikali inatarajia kuikamilisha mwaka 2022/23” amesema.