SHILINGI bilioni 100 zilizotolewa na Rais Samia zimeshusha bei za mafuta kuanzia bei mpya zitakazotumika kuanzia leo. Hivyo ndiyo inavyoweza kuelezwa kutokana na bei mpya zilizotangazwa jana.
Baada ya kupanda kwa mafuta yaliyoanza kutumika mwezi uliopita, serikali ilianza kuchukua hatua mbalimbali ili kupunguza makali ya bei za bidhaa hizo ikiwamo kutolewa kwa ruzuku ya Sh. bilioni 100.
Kutokana na hakli hiyo, hatimaye bei mpya za petroli na dizeli zilizotangazwa jana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) zimeshuka hali ambayo itawapa unafuu wananchi.
Taarifa iliyotolewa jana na EWURA ilibainisha kuwa bei hizo ni kwa shehena zinazoingia katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, alisema kwa Dar es Salaam, petroli imeshuka kwa Sh. 306 kwa lita; Mtwara Sh. 282 na Tanga kwa Sh. 152 mtawalia.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa petroli, Kaguo alisema dizeli imeshuka kwa Sh. 320 kwa lita kwa Dar es Salaam, Sh. 476 kwa Tanga na Sh. 486 kwa mafuta yanayoingia kupitia Bandari ya Mtwara.
“Kutokana na kushuka huko, kwa Dar es Salaam bei ya petroli kwa lita itakuwa Sh. 2,994 badala ya Sh. 3,301 kwa lita. Bei mpya ya dizeli itakuwa Sh. 3,131 badala ya Sh. 3,452 kwa lita,” alisema Kaguo.
Kwa mafuta yanayoshushwa kupitia Bandari ya Tanga, Kaguo alisema bei mpya ya petroli itakuwa Sh. 2,985 kutoka Sh. 3,137 wakati dizeli itakuwa Sh. 3,162 kutoka Sh. 3,639 kwa lita iliyokuwapo awali.
Aidha, katika Bandari ya Mtwara, alisema petroli itauzwa Sh. 2,979 kutoka Sh. 3,262 kwa lita wakati bei ya dizeli itakuwa Sh. 3,165 kutoka Sh. 3652 kwa lita.
“Bei hizi zilizotajwa hapa ni kwa ile miji ambayo bandari huzika zipo na shehena ya bidhaa hizo zinashushwa. Kwa hiyo hadi kufika kwenye miji husika kutoka kwenye eneo la bandari bei itakuwa inapanda kutokana na gharama za usafirishaji lakini kutakuwa na unafuu wa wastani wa bei zilizotajwa kutokea kwenye chanzo cha shehena,” alisisitiza Kaguo.
TPDC KULETA MAFUTA
Katika hatua nyingine, Kampuni ya Vitol Bahrain E.C imeshinda zabuni tatu za usafirishaji wa mafuta huku ikiwashangaza Wakala wa Serikali wa Uagizaji wa Mafuta ya Pamoja (PBPA) kwa zabuni ya mafuta ya nne ambayo itaisafirisha kwa bei sawa na bure.
Vilevile, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kwa mara ya kwanza limeshinda zabuni ya usafirishaji wa mafuta ya dizeli kuanzia Julai mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa PBPA na Mwenyekiti wa Kamati ya Zabuni ya Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja, Ali Saeed, alisema wamefungua zabuni ya Julai na wenye zabuni wamefika na kuingiza zabuni zao kwenye kasha na kufunguliwa hadharani.
Alisema kampuni saba zimeshiriki katika zabuni hizo na kampuni ya Tanzania iliyoshiriki ni TPDC na baada ya kutangazwa zabuni ya kwanza, kamati inachambua nyaraka kuhakiki kama imekamilisha masharti ya zabuni yenyewe.
Saeed alisema kama amekamilisha wanatangaza mshindi wa kiwango cha chini. Dizeli yenye ujazo wa 100,857 ambaye ameshinda Vitol Bahrain kwa bei ya chini na ametimiza vigezo vyote vya uagizaji wa mafuta kwa pamoja.
Mjumbe wa Kamati ya Kutathmini Zabuni, Paulo Runyalula, alisema tathmini inafanana na wastani wa mwezi uliopita, akifafanua: "Mafuta ya Julai yatakuwa wastani wa mafuta ya bei ya Juni, sasa tunachowashindanisha ni gharama za kusafirisha mafuta pamoja na faida yao."
Alibainisha kuwa washiriki walikuwa wanne: TPDC, Vitol Bahrain E.C, Agusta na Sahara, akisema: "Aliyeshinda kwa Dola za Kimarekani 46.4 ambaye ataleta tani 100,857 na tenda ya pili ya dizeli ameshinda Vitol Bahrain na tenda ya tatu ya dizeli ameshinda TPDC.
“Sasa hii kampuni ya Vitol Bahrain imeshinda zabuni ya nne gharama ya kusafirisha mafuta Dola za Marekani 0.05 kwa huo mzigo wa tani 100,857 utaletwa kama kwa Dola za Marekani 5,700, ni sawa na bure,” alisema.
WACHUMI WAFUNGUKA
Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Razack Lukina, alisema kushuka kwa bei ya mafuta kutapunguza ukali wa maisha kwa kuwa wafanyabiashara watashusha bei za vitu vilivyopanda kutokana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo.
"Wafanyabiashara walipandisha bei za bidhaa kwa sababu gharama za mafuta zilipanda. Kwa hiyo, kama kesho yanashuka, tunatarajia vitu vishuke bei. Siwezi kukuhakikishia hilo lakini ingetakiwa iwe hivyo," alisema.
Mchumi huyo aliitaka serikali kusimamia bei za bidhaa hizo kuhakikisha kuwa zinashuka kwa kuwa wafanyabiashara wanatabia ya kutoshusha bei hizo hata pale tatizo lililosababisha likitatuliwa.
"Ni 'nature' (asili) ya wafanyabiashara kutoshusha bei ya bidhaa sasa hapo serikali inatakiwa isimamie ili ishuke, ni suala la kuona bei kwanza inashuka kisha tutaona namna gani serikali itasimamia hilo," alisema.
Profesa wa Uchumi, Samwel Wangwe, alisema kushuka huko kwa bei ya mafuta kutachochea shughuli za maendeleo kwa kuwa mafuta yamekamata sehemu zote muhimu kwa maendeleo.
"Mafuta yanaingia kwenye sekta nyingi, kilimo kwenye matrekta, viwanda... Kwa hiyo, gharama zikiwa ndogo, sekta hizo zitajiendesha kwa wingi na hivyo kupunguza mfumuko wa bei. Bei nazo zikipungua ina maana mwananchi wa kawaida atamudu gharama za bidhaa," alisema.
*Imeandikwa na Beatrice Shayo na Jenifer Gilla