Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Salim Abdallah ‘Tray Again’ amesema klabu hiyo itamtangaza Kocha Mkuu mpya wakati wowote mwezi huu Juni 2022.
Simba SC ilitangaza kuachana na Kocha Mkuu Franco Pablo Martin mwanzoni mwa juma lililopita, baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba baina ya pande hizo mbili, kufuatia Kocha huyo kushindwa kufikia malengo.
‘Try Again’ amesema baada ya kutangazwa kwa Kocha Mkuu mpya, Simba SC itaanza zoezi la usajili ambao utapendekezwa na Benchi la ufundi, huku akiamini kufanya hivyo ndio njia sahihi ya kupata wachezaji watakaopendekezwa na kocha huyo.
“Usajili utafanywa na Kocha Mkuu mpya ambaye tutamtangaza wakati wowote kuanzia sasa, sisi viongozi tutashirikiana naye bega kwa bega ili kuhakikisha tunafanya jambo kubwa na kuwa na kikosi imara kuelekea msimu ujao.”
“Kocha atakua na wigo mpana wa kutuambia anahitaji wachezaji wa aina gani, tunaamini atakuja na vigezo vyake ambavyo ataviwasilisha kwetu kama viongozi, na sisi tutamtimizia atakachokihitaji.”
“Niwatowe wasiwasi Wanachama na Mashabiki wa Simba SC, tunakamilisha mchakato wa kumpa Kocha Mkuu mpya, na timu yao itaanza kususkwa kwa kiwango cha hali ya juu, ili tuweze kurudi katika makali yetu kama Simba SC ya miaka minne iliyopita.” amesema Try Again
Simba SC msimu huu imeshindwa kutetea mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, huku ikitolewa hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa changamoto ya mikwaju ya Penati dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini