SIMBA wanahitaji nini? Ni suala la kujiuliza kutokana na timua timua ya makocha ndani ya timu hiyo pamoja na kufanya vizuri katika misimu minne ya hivi karibuni.
Kwenye misimu hiyo makocha wote waliopita wameweza kutwaa mataji ya Ligi Kuu Bara na kuiwezesha timu hiyo kufika hatua ya robo fainali mara tatu mfululizo, lakini hakuna aliyemaliza misimu miwili.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ timua timua ndani ya timu hiyo ni kutokana na kushindwa kufikia malengo ya mikataba yao.
“Tumeondoa makocha wanne pamoja na mafanikio yaliyopatikana nafikiri sababu kubwa ni kushindwa kufikia malengo. Hatua ya robo fainali kwetu sio stori mpya tunahitaji nusu fainali jambo ambalo wameshindwa,” anasema Try Again.
“Mfano Pablo yeye ndiye kashindwa hata kutwaa taji la ligi na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ilikuwa ni lazima tuvunje mkataba wake. Kwanza alianza na kututoa hatua ya awali japo aliipeleka (timu) Shirikisho Afrika na kufika robo.”
Mwanaspoti linakuletea makocha waliopita ndani ya timu hiyo na rekodi zao tangu watue na kisha kutupiwa virago kutokana na kushindwa kufikia malengo.
PABLO FRANCO
Simba ilivunja mkataba na Pablo Franco baada ya kutoa taarifa hiyo kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo Instragram huku pia wakimtakia kila la heri kocha huyo kwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi na kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Kuondoka kwa Pablo kulikuja siku chache baada ya timu hiyo kuondoshwa kwenye hatua ya nusu fainali ya mashindano Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Baada ya kufikia makubaliano hayo hivi sasa kikosi cha timu hiyo kipo chini ya kocha msaidizi Sulemani Matola katika kipindi cha kumalizia msimu.
Pablo alitua nchini akichukua nafasi ya Mfaransa Didier Gomes Da Rosa aliyetimuliwa Oktoba 26, mwaka jana.
Mafanikio pekee ambayo Pablo anaweza kujivunia ni kuipa Simba ubingwa wa nne wa michuano ya Mapinduzi 2022, baada ya awali kutwaa taji hilo 2008, 2011 na 2015 kisha kuiwezesha kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika japo sio mara ya kwanza kufikia hatua hiyo.
DIDIER GOMES
Oktoba 26, 2021 timu hiyo ililiridhia ombi la aliyekuwa Kocha Mkuu, Didier Gomes Da Rosa kuachana kuanzia siku hiyo baada ya tathmini na majadiano ya kina na pande zote zikaafikiana kwa mujibu wa mkataba na manufaa ya wote.
Kuondoka kwa Gomes kulikuja siku chache baada ya timu hiyo kuondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana ilipokubali kichapo cha mabao 3-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Gomes alitua nchini akichukua nafasi ya Mbeligiji Sven Vandenbroeck ambapo alikiongoza kikosi cha Simba kwenye mechi 33 huku akishinda mechi 25, sare nne na kupoteza nne.
Kutokana na hatua hiyo aliyekuwa Kocha msaidizi wa timu hiyo, Thierry Hitimana ndiye aliyechukua mikoba ya Gomes akisaidiwa na Matola.
Gomes alikuja nchini siku chache baada ya Sven kuachana na vigogo hao Januari 7, kisha kutimkia Far Rabat ya Morocco saa chache tu baada ya kuiongoza Simba kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga FC Platinum ya Zimbabwe.
Gomes ambaye ni raia wa Ufaransa alikabidhiwa mikoba ya kuwanoa wababe hao wa Msimbazi na kilichofuata ni historia na rekodi bab’kubwa ndani na nje ya nchi akiwa na chama hilo ambalo linawatisha hata vigogo wa Afrika kwa sasa.
VANDENBROECK SVEN
Uongozi wa Simba uliachana na Sven ikiwa ni siku chache baada ya kushinda 4-0 katika Uwanja wa Mkapa dhidi ya FC Platinum kwenye Ligi ya Mabingwa na kusonga hatua ya makundi, na timu kuwa chini ya Matola kwa muda.
Aliondoka Simba ikiwa nafasi ya pili kwenye ligi baada ya michezo 15 na pointi 35 ikifungwa mbili na sare mbili, ikishinda 11 na kutimkia Far Rabat ya Morocco na Januari 24 Simba ikamtangaza Didier Gomes kama kocha mkuu akitokea El Merreikh ya Sudan.
PATRICK AUSSEMS
Aussems ambaye alichukua mikoba ya Mfaransa Pierre Lechantre alitokea kuwa kipenzi cha mashabiki wa Msimbazi tangu alipoanza kukinoa kikosi hicho na hata kufikia hatua ya kumpachika jina la utani la Uchebe.
Kocha huyo aliondoka akiwaachia mashabiki wa Simba kumbukumbu zenye msisimko wa kipekee, hasa ya kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/2019.
Aussems katika kipindi cha uongozi wake alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Pia mwanzo wa msimu huo alifanikiwa kutwaa Ngao ya jamii.
Hata hivyo, mafanikio makubwa ya Aussems ndani ya Simba ambayo ni vigumu kusahaulika ni kufika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Licha ya kupangiwa vigogo kutoka Kaskazini mwa Afrika, Simba haikupoteza mchezo hata mmoja katika uwanja wake wa nyumbani jijini Dar es Salaam, ingawa pia alipata changamoto ya kupoteza mabao mengi kwa mechi za ugenini.
Ikumbukwe kuwa katika kundi la Simba kulikuwa na vigogo kama AS Vita ya DR Congo, Al Ahly ya Misri, JS Saoura ya Algeria.
PIERRE LECHANTRE
Huyu ndiye kocha aliyeweka rekodi ya kuishi muda mfupi tu ndani ya Simba. Alianza kibarua Januari 2018 na ndani ya miezi sita aliondoka. Lakini tangu kuondoka kwa Milovan, Lechantre ndiye aliyekuja kuipa ubingwa kwa mara ya kwanza.
Aliifundisha timu kwa miezi sita tu na alitimuliwa kwa sababu mbalimbali. Kwanza kabisa ilitokana na kiwango kibovu kilichoonyeshwa na timu baada ya yeye kuanza kuinoa, lakini pia inadaiwa hata maelewano mazuri na msaidizi wake Masoud Djuma hayakuwa mazuri.
Pia ilidaiwa mshahara mkubwa aliokuwa akitaka aongezewe yakiwa ni baadhi ya mambo yaliyoanya kutimuliwa kwake.