MABAO mawili ya Pape Sakho na moja la Peter Banda yametosha kuipa Simba ushindi wa 3-0 mbele ya Mbeya City kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliomalizika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Simba ikiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Sakho kwa mkwaju wa Penalti dakika ya 37 baada ya kuchezewa madhambi na kipa wa Mbeya City, Haroun Mandanda.
Kipindi cha pili kilirejea kwa kasi ambapo timu zote zilishambuliana kwa zamu lakini mabeki wa pande hizo mbili walikuwa imara.
Simba ilipata nafasi ya kuongeza bao dakika ya 48 lakini mpira uliopigwa na Kibu Denis ulitoka nje ya lango la Mbeya City.
Dakika ya 55, Simba ilipata bao la pili kupitia kwa Sakho aliyepokea pasi ndefu kutoka nyuma na kuwatoka mabeki wa Mbeya City kabla ya kumchambua kipa Haroun Mandanda na kuujaza mpira nyavuni.
Dakika 60, Simba ilipoteza nafasi ya wazi ya kuandika bao lingine baada ya kiungo Mzambia Rally Bwalya kuchelewa kufanya maamuzi kabla ya mabeki wa Mbeya City kufika eneo la tukio na kuondosha mpira.
Wakati huo timu zote zilifanya mabadiliko, matatu kwa Mbeya City na matatu kwa Simba wakitoka Mzamiru Yassin, Sakho na Kibu na nafasi zao kuchukuliwa na Meddie Kagere, Yusuph Mhilu na Peter Banda.
Dakika ya 76 Simba iliandika bao la tatu kupitia kwa Banda aliyepokea pasi kutoka kwa Mohamed Hussein na kuachia shuti kali la chini chini lililomshinda kipa Mandanda na kujaa nyavuni.
Wakati huo huo Simba ilifanya mabadiliko mengine ambapo Rally Bwalya alikwenda benchi na nafasi yake kuchukuliwa na Thaddeo Lwanga.
Simba iliendelea kulisakama lango la Mbeya City lakini kuanzia dakika ya 80 kibao kiliwageukia ila uimara wa kipa Beno Kakolanya ukahakikisha hakuna bao linaingia.
Hadi dakika 90 zinamalizika Simba 3-0 Mbeya City na matokeo hayo yamewafanya Wekundu hao wa Msimbazi kufikisha alama 54 baada ya mechi 26 na kusalia nafasi ya pili huku Mbeya City ikibaki nafasi ya 10 na alama 32 baada ya michezo 27.