Sugu "Ana miaka chini ya 18 ni historia ya binti nilikutana naye usiku"



Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa HipHop, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu ameimba wimbo wa kwanza wa Ana miaka chini ya 18 kwenye The Dream Concert huku akieleza ni wimbo ambao aliutunga baada ya kukutana na binti akifanya kazi za usiku.

"Nilikutana naye nikamuuliza una umri gani, akasema miaka 17, nikamuuliza kwanini uko hapa? Historia aliyonipa ndiyo ilinisukuma niandike wimbo huu," amesema Sugu.

Huo ndio ulikuwa wimbo wa kwanza wa Sugu kuimba kwenye Dream Concert, tamasha maalumu la mwanamuziki huyo aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini la kuadhimisha miaka 30 ya muziki wake lililofanyika usiku wa kuamkia leo Jumatano Juni Mosi kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam

Akisikilizwa na wageni mbalimbali waliohudhuria tamasha hilo akiwamo mgeni rasmi, Rais Samia Suluhu Hassan, Sugu amesema safari ya muziki kwake ilikuwa na changamoto.


"Sina chuki na wadogo zangu ambao wanapiga pesa kwenye muziki sasa, kwani hata mimi sija lost, bado mimi ni taita," amesema Sugu katika tamasha hilo.

Mwana FA, Nikki wa Pili wateka jukwaa mbele ya Rais Samia

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Nickson Simon maarufu Nikki wa Pili na Mbunge wa Muheza (CCM), Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA wameungana na Sugu na wasanii wengine kuteka jukwaa walipoimba pamoja mbele ya Rais Samia kwenye tamasha hilo.


Huku akitabasamu, mshereheshaji alimuuliza Rais Samia amewaonaje vijana wake ambao ni viongozi kwenye Serikali yake wakipafomu?

Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na msanii wa muziki wa Hiphop, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ mara baada ya kuwasili Serena kwa ajili ya kuhudhuria tamasha la maadhimisho ya miaka 30 ya msanii huyo. Picha na Ikulu

Hata hivyo Rais Samia kwa muda huo hakujibu chote zaidi ya kutabasamu.

Baadaye wakati akitoa hutuba yake, Rais Samia aliweka wazi kuwa kuna kipindi alikuwa mtazamo kuwa mziki wa HipHop ni uhuni huku akieleza kuwa mtazamo huo umebadilika.


"Hata mimi nilipokuwa nikiwaona wanafoka foka niliona uhuni wakati ule, lakini kumbe sio kweli, muziki umeleta heshima," amesema.

Kuhusu wateule wake na wabunge ambao wako kwenye tasnia hiyo ya muziki, Rais Samia amebainisha kuwa hawezi kuwaingilia kwa kuwa wanaweza kujipanga katika kutimiza majukumu yao.

"Hapa wasanii wameimba sijasikia maneno ya kukera, nimeona wabunge na wakuu wa wilaya wakiimba, nikajiuliza wanafanya kazi saa ngapi, lakini wanajua wanavyojigawa, simvunji moyo, nimebariki aendelee tu," amesema Rais Samia.

Mtoto wa Dandu, Ruge wakumbukwa Dream Concert

Wadau wa Muziki wakiongozwa na Rais Samia wamesimama kwa muda kuwakumbuka wa wasanii na wadau wa muziki nchini waliotangulia mbele za haki.

Tukio hilo limefanyika kwenye tamasha hilo la The Dream Concert huku wakiwakumbuka Ruge Mtahaba aliyetangulia mbele za haki, Cool James 'mtoto wa Dandu' Mr Ebbo, Adili Kumbuka, Ranga, Cpwaa, John Walker na Complex ambao walitajwa kama wadau wakubwa wa muziki nchini huku picha zao na vipande vya baadhi ya nyimbo zao zikionekana kwenye skrini kubwa ndani ya ukumbi wa Serena linapofanyika tamasha hilo.

Rais Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kitabu cha Msanii Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ chenye jina la Muziki na Maisha from the Street katika Tamasha la Dream Concert lililofanyika Serena jijini Dar es Salaam. Picha na Ikulu

Pia, tamasha hilo limetumika kumuombea mwanamuziki na mbuge wa zamani wa Mikumi, Joseph Haule 'Profesa Jay' ambaye anaumwa kwa muda sasa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad