Tetesi za usajili zinazoongoza Klabu Ligi Kuu Bara



LIGI Kuu nyingi duniani zimemalizika, huku Tanzania ikiwa ni moja kati ya nchi chache ambazo bado hazijamaliza ligi yake. Hata hivyo, tayari tetesi za usajili zimeshaanza duniani kote, huku baadhi ya timu zikiwa zimeshaandaa wachezaji wakuwasajili kwa ajili ya msimu ujao.

Tayari Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limeshatoa taarifa kwa timu zote wanachama kuwa mwisho wa usajili kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ni Juni 30, mwaka huu na hakutokuwa na nyongeza ya muda.

Tanzania kama nchi zingine, pamoja na kwamba haijamaliza ligi yake, lakini tetesi za wachezaji kutoka nje ya nchi kuja kucheza soka la kulipwa tayari zimeanza. Lakini pia baadhi ya wachezaji kutoka klabu moja ya hapa kwenda nyingine nayo pia imeanza.

Kwenye makala haya tunakuletea wachezaji wa nje ya nchi na wa ndani ambao wamehusishwa kuwa watajiunga na klabu mbalimbali hapa nchini, twende sasa...

#1. George Mpole - Geita Gold

Ni straika ambaye yupo kwenye kiwango cha juu kwa sasa kwa kupachika mabao. Juzi aliifungia Taifa Stars bao kwenye mechi ya kutafuta tiketi ya kufuzu AFCON mwakani nchini Ivory Coast dhidi ya Niger.


 
Japo kuna taarifa kuwa ameongeza mkataba na timu yake, lakini timu kubwa za Simba, Yanga na Azam FC zimekuwa zikimtolea macho. Kwa sasa ana mabao 14 kwenye orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu sawa na Fiston Mayele wa Yanga.

Tetesi zinasema kuwa huenda akajiunga na moja kati ya timu hizo tatu kubwa. Pamoja na kuwa na mkataba na klabu yake, lakini timu za Simba na Yanga huwa hazishidwi kitu, linapokuja suala la usajili, hasa kwa mchezaji wa ndani.

#2. Victorien Adebayor - US Gendamarie

Huyu ni winga wa klabu ya US Gendamarie ya Niger, ambayo juzi alicheza dhidi ya Taifa Stars wakati Niger ikitoka sare ya bao 1-1 na Tanzania.

Ni winga machachari na alifanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika akiwa na timu yake hiyo. Anahusishwa mno kujiunga na klabu ya Simba, lakini pia ikidaiwa RS Berkane ya Morocco wameweka mzigo wa maana ili atue kwao.

Hata hivyo, mchezaji mwenyewe anaonekana kuwa na mapenzi na Simba, huku wakala wake akiwa na mapenzi na RS Berkane kutokana na kumuahidi pesa nyingi, iwapo dili hilo litakamilika.

#3. Shiza Kichuya - Namungo

Yupo kwenye kiwango kizuri msimu huu akiwa na timu yake ya Namungo, huku tetesi zikimhusisha kurejea kwenye klabu yake ya zamani, Simba.

Tetesi zinasema kuwa viongozi wa Simba wameamua kumrudisha ili hata kama wakiwa na winga mwingine kutoka nje wawe na kikosi kipana, ili kama akitoka mmoja, anayeingia awe anafanana na aliyetoka au kuwa na viwango visivyopishana sana.


 
#4. Stephane Aziz Ki - Asec Mimosas

Kiungo mshambuliaji huyu wa Klabu ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, raia wa Burkina Faso, awali alionekana kuwa kwenye rada za Simba.

Lakini baadaye ni kama viongozi wa Simba 'wakapotezea', na kwa sasa anatajwa kwenye tetesi za usajili ndani ya klabu ya Yanga. Naye pia alionekana kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, timu yake ikiwa kundi moja na Simba.

#5. Lazarous Kambole - Kaizer Chiefs

Ni straika raia wa Zambia ambaye mkataba wake unamalizika kwenye klabu ya Kaizer Chiefs, huku akihusishwa kujiunga na klabu ya Yanga.

Klabu hiyo inaonekana ni kama anaweza kuwa pacha wa Fiston Mayele, hasa kuelekea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

#6. Nathaniel Chilambo - Ruvu Shooting

Ni beki chipukizi ambaye yuko kwenye kiwango cha juu, akiichezea Ruvu Shooting kwa sasa. Tayari klabu kubwa zimeshaanza kumzengea, ambapo awali Simba ilionekana kama vile ingeweza kumsajili kirahisi, lakini baadaye Azam FC inasemekana imeongeza mzigo na sasa ipo kwenye hatua nzuri ya kupata saini yake.

#7. Cesar Manzoki - Vipers

Ndiye mshindi wa Kiatu cha Dhahabu kwenye klabu ya Vipers ya Uganda, akiipa ubingwa pia timu hiyo.

Raia huyu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, anatajwa kuwa atavaa jezi nyekundu na nyeupe msimu ujao wa ligi akiwa na klabu ya Simba.

#8. Pascal Wawa - Simba

Ni mmoja wa wachezaji wanaodaiwa kuwa huenda watatemwa na klabu ya Simba mwishoni mwa msimu huu.

Tetesi zinasema kuwa klabu iliyopanda daraja msimu huu Singida Big Stars FC inamnyemelea raia huyu wa Ivory Coast na huenda akaitumikia msimu ujao wa Ligi Kuu.


 
#9. Saido Ntibazonkiza - Yanga

Siku chache tu baada ya kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu, klabu ya Yanga pia ikatangaza kuachana na kiungo mshambuliaji huyo raia wa Burundi.

Klabu ya Singida Big Stars FC, ndiyo tetesi zinasema ipo kwenye nafasi nzuri zaidi ya kumnyakua pamoja na kwamba Azam FC nao wanamtolea macho.

#10. Moses Phiri - Zanaco

Ni straika raia za Zambia ambaye tetesi zinadai ameshamalizana na klabu ya Simba. Zipo tetesi zinasema kuwa Simba ilitaka kumsajili kipindi cha dirisha dogo, lakini klabu yake ya Zanaco iligoma, na kudai haitaweza kumtoa kutokana na kumtumia kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Habari zinasema kuwa baada ya kumkosa, ilibidi wampe mkataba wa awali. Inaonekana ndiye chaguo namba moja kwa Simba msimu ujao wa ligi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad