TFF nendeni na ratiba CAF, Simba, Yanga mulikeni usajili



MSIMU wa Ligi Kuu Bara 2021/22, umebaki raundi nne kwa kila timu kabla ya kumalizika ifikapo Juni 29, mwaka huu, ambapo klabu zote 16 shiriki zitakuwa zimecheza mechi 30 kila moja na baada ya hapo ndipo dirisha rasmi la usajili kuelekea msimu mpya litafunguliwa.

Kumalizika kwa msimu pia, huwezesha kujulikana kwa timu zitakazoiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa, inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF; yaani Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Kama ilivyokuwa msimu uliopita, ujao pia Tanzania imepata nafasi ya kuwakilishwa na timu nne, mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho Afrika.

Ikumbukwe pia bingwa wa Ligi Kuu na mshindi wa pili, ndio hubeba dhamana ya nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa wakati timu itakayoshika nafasi ya tatu na ile itakayotwaa Kombe la Shirikisho la Soka nchini (FA Cup), ndizo hukata tiketi ya kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Hivyo, wakati Ligi Kuu ikitarajiwa kumalizika Juni 29 huku fainali ya Kombe la FA ikitarajiwa kuchezwa Julai 2, mwaka huu, michuano ambayo itatoa wawakilishi wetu wa nchi kimataifa, tayari CAF imepuliza kipenga cha siku ya kufungwa kwa dirisha lake la usajili wa wachezaji na klabu zitakazoshiriki michuano yake hiyo miwili.


 
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, dirisha hilo litafungwa Juni 30, mwaka huu siku moja baada ya kumalizika Ligi Kuu Bara na siku tatu kabla ya fainali ya Kombe la FA nchini, ambalo hutoa mwakilishi wetu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Hivyo, kutokana na Kalenda ya TFF, hadi tarehe hiyo ya kufungwa kwa dirisha la usajili la CAF, itakuwa haijajulikana mwakilishi wa nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwani fainali ya FA Cup kati ya Yanga na Coastal Union itapigwa Julai 2, jambo ambalo linahitaji marekebisho ya haraka ili kuendana na kalenda hiyo.

Ni wazi presha kubwa itakuwa kwa upande wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwani Yanga ambayo inacheza fainali ya FA, tayari ina tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa sambamba na Klabu ya Simba.


Yanga hadi sasa ina pointi 64 kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu huku ikifuatiwa na Simba yenye alama 51, pointi ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika ligi hiyo kwa sasa, kwa maana hiyo vigogo hivyo vya nchi moja kwa moja vina tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Kinachotakiwa kwao kwa sasa ni kuanza kuingia makubaliano na wachezaji wanaotaka kuwasajili na kusaini mikataba ya awali baada ya pande zote kukubaliana ili ligi tu itakapokamilika kukamilisha mchakato huo wa usajli na kuwahi kuwasilisha majina ya nyota wao CAF kabla ya dirisha kufungwa.

Lakini pia ni wakati wa TFF na Bodi ya Ligi kujichimbia na kufanya marekebisho ya ratiba haraka ili Ligi Kuu imalizike katikati ya mwezi huu kuwezesha wawakilishi wa nchi kwenye michuano ya CAF kujulikana pamoja na dirisha la usajili kufunguliwa mara moja.

Kadhalika, hatuoni sababu ya fainali ya FA kupigwa Julai 2, wakati inaweza kufanyika mapema hata kabla ya Ligi Kuu kumalizika ili kutoa nafasi kwa mshindi kujipanga kwa michuano hiyo ya CAF hasa ukizingatia timu ambazo hupata nafasi hiyo nyingi husumbuliwa na ugeni wa mashindano hayo pamoja na uwezo kiuchumi.


 
Tunatambua baada ya dirisha hilo la CAF kufungwa hutolewa wiki mbili kwa klabu kuomba kufunguliwa kufanya usajili lakini kwa kulipia, hivyo kama timu hazitafanya usajili wao mapema, ikiwa ni pamoja na TFF kuhakikisha ligi inamalizika mapema zaidi, kutazigharimu sana klabu zetu ambazo baadhi kiuchumi hazipo vizuri.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad