TMA yatahadharisha Baridi kali Nyanda za Juu kusini


Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mwelekeo wa kipupwe unaotarajiwa kuanza Juni hadi Agosti mwaka huu katika mikoa mitano ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Magharibi yenye miinuko, inatarajiwa kuwa baridi kali chini ya nyuzi joto nne (4 °C) .


Mkurugenzi wa Huduma za Utafiti na Matumizi wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, akiitaja mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro, kuwa itaathiriwa na hali hiyo.


Lakini DK Chang’a alisema hali ya joto kiasi na baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo mengi nchini.


Alisema kiwango cha baridi katika maeneo hayo kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 4 hadi 14, huku maeneo yenye miinuko yakitarajiwa chini ya nyuzi joto nne.


Akizungumzia Mkoa wa Ruvuma, Dk Chang’a alisema unatarajiwa kuwa na baridi kiasi cha nyuzi joto kati ya 6 C na 14 C, Mtwara na Lindi kati ya nyuzi joto 14 C na 22 C, Singida na Dodoma nyuzi joto 12 C na 18 C, Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma nyuzi joto 14 C na 18 C.


Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara inatarajiwa kuwa na nyuzi joto kati ya 10 C na 18 C, Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kaskazini Morogoro, Unguja na Pemba nyuzi joto 18 C na 26 C wakati Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu ikitarajiwa kuwa nyuzi joto kati ya 14 C na 20 C.


“Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi nchini na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani inatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Pwani Kaskazini pamoja na nyanda za juu kaskazini mashariki na vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza kati ya Juni na Julai,” alisema Dk Chang’a.


Pia, alisema katika kipindi cha Juni na Agosti vipindi vya upepo mkali vinatarajiwa kuvuma kutoka kusini mashariki na mashariki (Matlai) katika ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na meneo ya nchi kavu, hususan Agosti mwaka huu.


Dk Chang’a alisema athari zinazoweza kujitokeza ni homa ya mapafu kwenye mifugo na binadamu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad