Tozo miamala ya simu zaongeza Pato la Taifa



 
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema thamani ya miamala ya fedha kwa njia ya simu imeongeza Pato la Taifa.

Dk. Nchemba alitoa kauli hiyo jana alipohutubia kwa njia ya mtandao wakati akifungua mkutano wa 10 wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) unaofanyika jijini Arusha kwa ushirikiano na Jumuiya ya Kimataifa ya Huduma Jumuishi za Fedha (AFI), ukishirikisha viongozi wa jumuiya hiyo Ukanda wa Afrika (AfPI).

Alisema thamani ya miamala hiyo imeongezeka kutoka asilimia 40 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 66 mwaka 2021, huku watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu za kiganjani ikifikia milioni 35.3 mwezi Desemba mwaka jana, sawa na asilimia 61 ya watu wote nchini.

“Hapa mtajadiliana, natumaini mtabadilishana uzoefu juu ya namna ya kufanya sekta ya fedha barani Afrika kuwa ya kidijitali zaidi, kiasi kwamba tunahamia kwenye jumuiya ya watu wenye fedha kidogo ikiwa si jamii isiyo na fedha taslimu.

"Hatua hii siyo tu itakuza ushirikishwaji wa kifedha na maendeleo ya kiuchumi, bali itasaidia kudhibiti ufisadi, mtiririko wa fedha haramu, kuongeza uwazi na kuboresha ukusanyaji wa mapato ya serikali," alisema.


 
Gavana wa BoT, Prof. Florens Luoga, ambaye ni Mwenyekiti wa AfPI, alisema suala la utakatishaji wa fedha limeathiri nchi za Afrika ikiwamo Tanzania na kusababisha dola zaidi ya bilioni 350 za Marekani kupotea kila mwaka.

“Kama tungechukua hatua zaidi kudhibiti utakatishaji wa fedha, upotevu huu ungeshuka hadi Dola bilioni 10 za Marekani,” alisema.

Gavana alisema katika kukabiliana na utakatishaji huo wa fedha, kuna timu maalum barani Afrika kupitia umoja huo inayofanya kazi chini ya aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, kudhibiti suala hilo na kuwa kila nchi inachukua hatua ya kudhibiti hilo.


Akizungumzia kuhusu mkutano huo unaojumuisha magavana, manaibu wao na wataalamu wa benki kuu kutoka nchi 30 za Bara la Afrika na wadau mbalimbali wa masuala ya kifedha, Prof. Luoga alisema umelenga kuhakikisha huduma jumuishi za kifedha zinawafikia wananchi wa ngazi zote.

“Katika mkutano huu wa 10 ambao kwa miaka miwili mfululizo tulikuwa hatujakutana ana kwa ana kutokana na janga la UVIKO-19, tunakutana kujipima na kuangalia changamoto katika kutoa huduma jumuishi za fedha kwa wananchi wa kawaida," alisema.

Prof. Luoga alisema katika mkutano wa mwaka huo, watajadili utoaji wa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao na kuona iwapo zinaleta athari kwa wananchi, kuangalia jinsi ambavyo mtoa huduma na mpata huduma watakavyotambuana bila kuleta madhara na kubadilishana uzoefu wa kupata ufumbuzi wa pamoja wa huduma ya teknolojia.

Alisema kwa upande wa Tanzania, BoT imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kifedha umbali usiozidi Km 15, lengo likiwa ni kuhakikisha huduma za kifedha zinabadilisha maisha ya wananchi.


 
"Gharama za huduma mtandao hapa kwetu ni kweli ziko juu, lakini Benki Kuu inaendelea kuweka kanuni mbalimbali ambapo tumeshaanzia kwenye benki ambapo tumepunguza gharama," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa AfPI, Dk. Alfred Hannig, alisema tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo mwaka 2013, msingi wake ni kusaidia maendeleo ya sera za huduma jumuishi na mipango ya udhibiti.

Alisema kuna haja ya kulinda maslahi ya Afrika katika mijadala ya dunia na kuhakikisha usawa katika mijadala na ushirikishwaji stahiki katika jukwaa la dunia.

Alisema wataendelea kuwasiliana na bodi za uwekaji viwango (Standard Setting Bodies) kuhakikisha viwango vilivyowekwa havififishi mafanikio yaliyopatikana katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha barani Afrika.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad