WALE ndiyo Yanga katika ubora wao. Unaweza kuwakataa mdomoni lakini moyoni unajua kabisa shughuli yao huwa haiwi ya kitoto. Wanapoamua kufanya shughuli yao, huifanya kwa asilimia zote. Ni kama ambavyo waliamua kuifanya shughuli yao ya kusherekea ubingwa jumapili iliyopita.
Nani aliamini kwamba Yanga wanaweza kufanya gwaride la kuvutia namna ile? Vile ndivyo namna ambavyo Klabu za Ulaya hufanya. Wanapotwaa ubingwa, huzunguka katika miji yao na kusherekea pamoja na mashabiki wao.
Majuzi tu Liverpool walifanya gwaride baada ya kupoteza fainali ya UEFA. Walifanya gwaride kusheherekea ubingwa wao wa kombe la ligi (Carabao Cup) na kombe la FA. Nafikiri Liverpool waliamua kuchelewesha gwaride lao ili wajumuishe pamoja na sherehe za ubingwa wa klabu bingwa Ulaya kama wangeupata. Bahati haikuwa upande wao na shilingi ililala upande wa Real Madrid.
Liverpool wakafanya gwaride na mataji yao mawili ya ndani. Bado mashabiki walijitokeza sana na kukatiza kibabe mitaa ya Walton yalipo makao makuu ya Everton, kama ambavyo Yanga walikatiza mtaa wa Msimbazi.
Kuna kitu kimoja Yanga walikipatia sana. Lile wazo la kuamua kwenda kukabidhiwa kombe Mbeya liliwasaidia vitu viwili vya msingi.
Kwanza waliwaweka karibu mashabiki wa mkoani na kuwaonesha nao kwamba wana thamani sawa na wale wa Dar es Salaam. Mashabiki wa mikoani hawapati sana bahati ya kushuhudia matukio pamoja na mechi adimu za klabu zao.
Siku ya mwananchi, mechi ya ligi dhidi ya mtani na mechi zote za kimataifa hufanyika Dar es Salaam. Mikoani huwa wanapata kwa nadra sana matukio kama haya. Kwahiyo Yanga kukubali kwenda mkoani kukabidhiwa kombe, ni kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya klabu na mashabiki wa mkoani waliosahaulika.
Kitu cha pili ni kiu waliyowatengenezea mashabiki wa Dar es Salaam. Kwa Yanga ilikuwa rahisi kupanga njia watakazopita kutokea Uwanja wa Ndege kwasababu lazima mashabiki wangewasubiri kwa ajili ya kulipokea kombe hata kama kusingekuwa na gwaride. Hali ingekuwa tofauti kidogo kama wangekabidhiwa lile taji Dar es Salaam. Ingekuwa ngumu kukusanya mashabiki kisha kuzunguka nao mitaani ukizingatia ukweli kwamba tayari walikwisha kuliona taji Uwanja wa Mkapa.
Mpango wa kupokelea kombe Mbeya uliwapa kiu mashabiki wa Dar es Salaam na kurahisiha ratiba ya mzunguko wa Yanga.
Lakini kuna ukweli kwamba mashabiki wa Yanga huwa wanaipenda sana timu yao linapokuja suala la kufika katika matukio ya klabu.
Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi Tanzania, msimu uliotamatika Yanga ndiyo timu iliyoingiza mashabiki wengi uwanjani. Hapo kumbuka Yanga hawakuwa na timu imara sana na kwa jinsi fulani walikuwa wanyonge kwa Simba. Lakini bado walifika katika mechi zao kuliko wengine.
Ni kama ambavyo walikuwa wanafika uwanja wa ndege kuwapokea mastaa wa timu yao kabla msimu haujaanza. Wakiwa hawafahamu hata ubora wa kina Michael Sarpong, bado Yanga walimiminika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere kuwapokea mastaa wao wapya.
Rejea namna Yanga walivyoshiriki wiki ya wananchi na mechi ya watani ambayo Yanga alikuwa mwenyeji, kwa namna fulani Yanga walifunika kuliko ndugu zao Simba.
Ni sababu hii inayofanya niamini kwamba mashabiki wa Yanga wanaipenda sana timu yao. Kitu pekee ambacho huwa wanaanguka ni katika michango.
Huu upendo huwa unawapa deni wachezaji wa Yanga na kujikuta wakijituma isivyokuwa kawaida wanapoichezea Yanga. Haishangazi kuona wachezaji wanaojituma sana kama Shomari Kibwana husemekana ni wachezaji waliokaa ki-yanga-yanga. Ni madeni wanayobeba mioyoni mwao kutoka kwa mashabiki.
Ndiyo maana hata miaka miwili iliyopita Yanga wakiwa katika kilele cha ubovu wao, bado walifanikiwa kumaliza ligi juu ya Azam FC. Ni kwasababu ya kujituma kwa wachezaji wao.
Hili gwaride la Yanga linaacha deni kwa bingwa wa ligi kuu ajaye. Najua Simba watakua wameumia na kichini-chini watakuwa wakiuma meno kwamba ‘ngoja zamu yetu ifike, tutawakomesha.’ Simba watatamani kufanya zaidi ya Yanga, kwani wameshawahi kuacha kushindana? Yanga nao watatamani kubeba tena ili kuzidi kuwadhoofisha Simba. Nafikiri, tunaweza kuwa na msimu mgumu sana msimu ujao.
Ngoja leo msimu umalizike, tuone itakavyokuwa msimu unaofuata.