Kasoro ya Kenya kisiasa mpaka sasa ni ukabila na ukanda. Mathalan, mwaka huu baada ya Wakikuyu kutokuwa na mgombea urais mwenye nafasi ya kushinda, kulitokea ulazima wa mgombea mwenza.
Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya Coalition na William Ruto, mwenye tiketi ya United Democratic Alliance (UDA), ndio vinara wa mbio za urais na wote wagombea wenza wao ni Wakikuyu kutoka Kanda ya Kati (Mlima Kenya).
Kwamba ilibidi Raila wa Nyanza na Ruto anayetokea Rift Valley, wafanye machaguo yenye kuwaridhisha Wakikuyu ili kujenga ushawishi mkubwa Mlima Kenya. Raila mgombea mwenza wake ni Martha Karua, Ruto yupo Rigathi Gachagua.
Shida kubwa ya Kenya ni kuwa ngome za kisiasa zinaundwa kwa nguvu ya ukabila na kanda. Yaani ukitaka kura za Wakamba lazima ubebwe na ‘samaki mkubwa’ wa ukambani, Kalonzo Musyoka ambaye ni Mkamba.
Unapohitaji kujizolea kura nyingi kwa waswahili wa Pwani, omba mkono wa mswahili Hassan Joho. Hiyo ni hali halisi katika maeneo mengine. Na hilo ndilo tatizo kuu la Kenya. Waluo na Mluo, Wakikuyu kwa Mkikuyu, Wakalenjin na Mkalenjin, na kadhalika.
Tanzania ilishavuka hilo eneo miaka mingi. Kabla ya uhuru, baada ya Tanganyika kuwa dola huru na hata ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hakuna ‘uzuzu’ wa kupiga kura kikabila, wala kikanda. Shukurani nyingi kwa Mwalimu Julius Nyerere kwa kuufanya ukabila kuwa hauna maana mbele ya Utanzania.
Ukiacha ukabila, Kenya wanaipa somo Tanzania kuhusu namna bora ya kuzielekea siasa katika nchi za dunia ya tatu; kufuta ukiritimba wa vyama na kubebwa na mambo mawili ambayo ni haiba na agenda.
Kenya leo haiangalii ni chama gani kinagombea, anatazamwa mgombea, vilevile agenda anayobeba kwenye uchaguzi. Tanzania bado watu wanakumbatia vyama vya siasa kama dini. Huu ndio “ushamba wa kisiasa” usiotakiwa.
Pamoja na Kenya wameshavunja dari ya kioo katika siasa za ukiritimba wa vyama, bado zama mpya zinabebwa na masilahi binafsi kuliko muktadha wa kesho njema ya taifa hilo.
Mathalan; Kalonzo amelazimika kubaki Azimio la Umoja na kumpigia kampeni Raila kwa kuwa hana pa kwenda na ana ahadi ya kuteuliwa kuwa Waziri Kiongozi. Vilevile, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula, wapo na Ruto kwa sababu ya nafasi za uongozi.
Ukiacha hilo, Wakenya wapo kwenye nyakati bora za kuifundisha dunia ya tatu kuwa vyama ni majukwaa tu ya kusaka dola na uongozi wa kisiasa. Mtu akija kuomba nafasi ya kuongoza, apimwe kwa agenda yake, rekodi zake kama zipo au historia yake.
Siasa za “chama chetu ndio mwarobaini wa matatizo”, hazina uhalali. Zimepitwa na wakati. Agenda ya wakati husika pamoja na aina ya wagombea, ndio mauzo yanayotakiwa sokoni.
Tanzania bado imekumbatia siasa za kiitikadi mithili ya dini. Kama ambavyo kila dini itakuja na ushawishi kuwa yenyewe ndio njia sahihi ya kwenda peponi, kadhalika vyama. Kila kimoja kinajenga ushawishi wa jumla kuhusu kesho ya nchi.
Uongozi mzuri haujengwi na propaganda za nchi ya ahadi, palipo na mito yenye asali na maziwa, bali huundwa kwa agenda na haiba ya mtu katika kutafsiri nadharia kwenda vitendo kiuongozi.
Kenya inafundisha kuwa sura ya leo kisiasa isikuongopee, ya kesho huyajui. Raila alipambana miaka 20 na Rais Uhuru Kenyatta, lakini leo wapo pamoja.
Ruto alikuwa ‘patna’ wa Uhuru katika safari ya urais, ila kuelekea Uchaguzi Mkuu Kenya unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, mwaka huu, kila mmoja ameshika njia yake.
Mwaka 2002, Raila aliongoza vuguvugu la kuibomoa Kanu, kwenda kuunda Narc, sababu ikiwa kumkataa Uhuru kugombea urais. Raila akasimama na Mwai Kibaki dhidi ya Uhuru. Kibaki alishinda.
Mwaka 2007, Uhuru alimuunga mkono Kibaki kwa nguvu kubwa, aliyekuwa anashindana na Raila. Safari hiyo, Ruto alikuwa bega kwa bega na Raila. Wakati mwaka 2002, Ruto alimpigania Uhuru kwa nguvu kubwa.
Mwaka 2007, Ruto na Uhuru walinyukana, kila mmoja akimtaka wa kwake ashinde, damu ikamwagika Kenya.
Mwaka 2013, Uhuru na Ruto wakawa kitu kimoja dhidi ya Raila, ikawa hivyohivyo mwaka 2017. Baada ya miaka 20, Uhuru yupo kwenye maombi akiwataka Wakenya kumchagua Raila, kwani ndiye kiongozi anayewafaa na sio Ruto, aliyeshirikiana naye kuongoza serikali kwa miaka tisa.
Tanzania bado kuna siasa za watu kuitana wasaliti baada ya kutofautiana. Kenya imeshavuka huko.
Usije kustaajabu miaka mitano ijayo, Uhuru akasimama jukwaani kumwombea kura Ruto. Itategemea na mazingira ya wakati husika.
Imewezekana kwa Raila na Uhuru kuunganishwa na Mpango wa Kujenga Daraja la Maridhiano (BBI), haitashindikana siku Uhuru na Ruto watarejea mezani na kusafiri pamoja kutokana na agenda ya wakati husika.
Wakenya wameshavuka siasa za ubinafsi wa vyama na sasa wanaamini katika “umoja ni nguvu”. Raila na Ruto, wamehakikisha wanajenga kambi zenye kuviweka pamoja hadi vyama vidogo kabisa. Ni kwa sababu umoja ni nguvu.
Tanzania, bado kila chama kinataka king’ang’ane chenyewe kwenye uchaguzi. Kishinde ili kimiliki kila kitu kwenye dola.
Kisichangie madaraka na vyama vingine. Kingine kibebe kambi ya upinzani, kitambulike kama kinara wa upinzani.
Wakenya walishajifunza. Uchaguzi Mkuu mwaka 1992 na 1997, Rais Daniel arap Moi, alishinda kwa sababu wagombea na vyama vingine, walishiriki kwa dhamira ya kutaka kushinda. Wakagawa kura, Moi akashinda kiulaini.
Kenya ilifanya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992. Waliochuana kugombea urais walikuwa nane. Hata hivyo mechi ilikuwa ya wanne, waliosalia walisindikiza.
Moi (Kanu), alivuna asilimia 36.35, akashinda uchaguzi. Kituko ni kuwa Kenneth Matiba (Ford Asili), Mwai Kibaki (DP) na Jaramog Odinga (Ford Kenya), walipata kura jumla asilimia 62.9.
Hivyo, kama Matiba, Kibaki na Jaramog wangeungana dhidi ya Moi, pengine Moi asingeibuka mshindi. Kwa kuwa wagombea wa upinzani walitaka kila mmoja aoneshe msuli wake, ikawa nafuu kwa Moi.
Kama ulivyo msemo wa kuvuja kwa pakacha, mwaka 1997, wapinzani waliingia kwenye uchaguzi wakiwa wamesambaratika.
Moi akishinda uchaguzi kwa kupata kura asilimia 40. Wakati wapinzani, Kibaki, Raila Odinga, Michael Wamalwa na Charity Ngilu, walivuna kura asilimia 58.14.
Mwaka 2002, wapinzani walipoungana Narc, Kanu ikaondolewa madarakani. Mwaka 2007, ilijenga picha ya umuhimu wa kuungana, kisha mwaka 2013, siasa za Kenya zimetengeneza ‘fasheni’ ya ushirikiano wa vyama kuelekea uchaguzi.
Vyama sio dini, ni majukwaa ya kusaka uongozi na dola. Nyakati hizi ambazo vyama havizungumzi itikadi, isipokuwa agenda, Kenya inapaswa kuwa mwalimu mzuri.
Hasa vyama vya upinzani. Kutengeneza agenda na kuunganisha nguvu ili kuvuna matunda ya haiba za kila upande.