Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, Juni 22, 2022 inatarajia kutoa uamuzi juu ya zuio la kisheria dhidi ya kuondolewa kwa wamasai katika maeneo yao, huku wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa (UN), wakieleza hofu yao juu ya madai ya kumegwa kwa ardhi ya asili ya wamasai katika eneo la Loliondo lililopo Mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa ya wataalamu tisa iliyotolewa jijini Geneva Uswisi Juni 15, 2022, imesema kitendo kinachoendelea eneo la Loliondo kinakosa uwazi na mashauriano baina ya Serikali na jamii ya wamasai, katika upangaji wa mipango na uamuzi na kuamua kuvihusisha vikosi vya ulinzi na usalama kulinda eneo lao hilo la kiasili.
“Tuna wasiwasi mkubwa na ripoti za vikosi vya usalama vya Tanzania kutumia risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi tarehe 10 mwezi huu wa Juni, kitendo kinachoripotiwa kusababisha watu takribani 30 kupata majeraha madogo na wengine makubwa sambamba na kifo cha afisa mmoja wa polisi,” wamesema wataalamu hao.
Wamesema, Juni 6, 2022 baada ya mashauriano ya faragha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela alitangaza uamuzi wa kugeuza eneo la ukubwa wa kilometa 1,500 za mraba kutoka eneo la kilometa 4,000 za mraba la ardhi ya vijiji linalojumuisha eneo la pori tengefu la Loliondo, kuwa pori tengefu.
Wataalamu hao wamesema mabadiliko hayo yanamaanisha kuwa wakazi 70,000 wa vijiji vya Ololosokwan, Oloirien, Kirtalo, na Arash villages,watalazimika kuhama.
Wakizungumzia eneo la Ngorongoro wamesema, “tuna hofu juu ya mipango ya Tanzania ya kuhamisha wamasai 150,000 kutoka eneo la hifadhi la Ngorongoro pamoja na Loliondo bila ridhaa yao au kujulishwa na kuamua kwa mujibu wa sheria za haki za kibinadamu za kimataifa.”
Katika hoja zilizojibiwa kwenye Mkutano wa 50 wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa, jijini Geneva, Uswisi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa wa Geneva, Balozi Hoyce Temu amesema Serikali na wakazi wa Loliondo walijadiliana na kukubaliana kuwa kati ya kilometa za mraba 4,000 zilizopakana na vijiji 14, kilometa za mraba 2,500 zitumiwe na vijiji vya karibu kwa kujikimu kimaisha
“Baada ya serikali na jamii ya wakazi wa Loliondo kujadiliana na kukubaliana, kuwa kati ya kilometa za mraba 4,000 zilizopakana na vijiji 14, ilikubaliwa kuwa kilometa za mraba 2,500 zitumiwe na vijiji vya karibu kwa kujikimu kimaisha, na kilometa za mraba 1,500 ziwe kwa ajili ya uhifadhi chini ya serikali ya Tanzania au kwa jina jingine iwe pori tengefu,” amefafanua Balozi Temu.
Amesema, alama za mipaka zimeanza kuwekwa kwenye pori hilo tengefu la Loliondo, lakini watu wachache wenye nia mbaya ya mpango wa Serikali ya Tanzania wa kuwapatia maisha bora wakazi wa Loliondo na kuendelea kuhifadhi eneo hilo kwa maendeleo endelevu, walianza kuandamana na kupinga mpango huo.
Balozi Temu amesema “katika hatua hiyo, baadhi ya waandamanaji walichukua picha na kuchanganya na picha ambazo hazikuwa za eneo hilo na Serikali ilitoa wito kwa wale wanaodai kuumizwa ili sheria ichukue mkondo wake, lakini hakuna aliyejitokeza na wananchi wa Loliondo wanaendelea na maisha yao kawaida na kwa amani.”
ABalozi Hoyce Temu amesisitiza kuwa Serikali itaendelea na majadiliano kuhakikisha wananchi wananufaika kiuchumi na kijamii na wawe na haki katika kufaidi ardhi yao.
Mwaka 2010, eneo la hifadhi ya ya Taifa ya Ngorongoro, lilitambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kuwa eneo la urithi wa dunia.