KUMEKUCHA Jangwani. Vita ya nafasi ya Urais wa Yanga imeanza. Kuna majina makubwa kwa mashabiki na wanachama ambayo kabla kesho Jua halijazama yatapishana kuchukua fomu za nafasi hiyo.
Tayari ratiba ya uchaguzi huo chini ya Mwenyekiti, Malangwe Mchungahela inaonyesha zoezi hilo la kuchukua fomu litafikia tamati kesho Juni 9 likianzia Juni 5 na uchaguzi unafanyika Julai 10 mwaka huu.
Hatua ambayo itawaibua wagombea wengi leo na kesho kupishana kuziwahi fomu hizo ingawa baadhi walipanga kufanya kama sapraizi kwani siku nyingi hawajaonekana Jangwani.
Mwanaspoti limebaini kuna vikao vingi vinaendelea jijini Dar es Salaam vya kupanga mikakati huku baadhi ya wanaopanga kuchukua fomu wakitanguliza wapambe matawini kupima upepo lakini wanachunguza chini chini kujua nani mwenye nia ya kugombea hasa nafasi ya urais.
Karata hizo zinachezwa kiakili na kuna majina makubwa sita ambayo yanaviziana kuchukua fomu kuwania kiti hicho ingawa baadhi yao wapambe wao wameanza kuwanadi chinichini na kuhamasishana kujaa Jangwani siku ya kuchukua fomu.
Dk Mshindo Msolla amewaambia watu wake wa karibu lazima awanie tena kuendeleza mafanikio yake ya msimu huu.
Hata hivyo, Msolla atakuwa na vita nzito kutokana na majina mengine matano ambayo nayo yanakitaka kiti hicho ambayo yanaushawishi mkubwa kwa wanachama watakaopiga kura.
SEIF AHMEID
Hajasikika kwa kitambo kidogo Yanga lakini Seif Ahmeid ‘Seif Magari’ yumo. Kinara huyu ambaye alikuwa kwenye kamati ya mashindano inayokwenda kurudisha mataji alikuwa pacha wa Abdallah Bin Kleb katika kuisimamisha Yanga kwenye utawala wa Yusuf Manji, ambaye atachukua fomu kwa ushawishi wa makundi ya wanachama wa klabu hiyo.
HERSI SAID
Mhandisi Hersi Said ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, baada ya kuiwezesha Yanga kupitia nafasi yake ndani ya GSM na kamati ya mashindano sasa anataka kiti cha urais wa klabu hiyo na wakati wowote kuanzia leo atatua kuchukua fomu, Mwanaspoti limejiridhisha pia kutoka ndani ya klabu hiyo.
DAVIS MOSHA
Mosha ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga katika utawala wa Manji pia hivi karibuni msimu huu amekuwa akisafiri sehemu mbalimbali kuipa nguvu Yanga nyumbani na ugenini.
Mosha kama ilivyo kwa Seif anashawishiwa kwa kiasi kikubwa na makundi ya wanachama ambao wamemuahidi sapoti na kura za Urais na ameonyesha kuridhia ila ataibuka kama sapraizi.
ATHUMANI KIHAMIA
Mtu mzito mwingine ni Athuman Kihamia ambaye ni Katibu tawala wa Mkoa wa Arusha akiwa pia kwenye Kamati ya Utendaji ya Yanga naye yumo katika vita hiyo, akipima upepo wa jinsi ya kuchukua fomu hiyo kwa kushtukiza.
ABBAS TARIMBA
Tarimba Abbas maarufu kwa jina la Thabo Mbeki ambaye ndiye muasisi wa mchakato wa mabadiliko akifanya hivyo miaka mingi nyuma naye anapiga hesabu za kuchukua fomu hiyo wakati wowote kuanzia leo akizidi kuweke ugumu wa kiti hicho.