Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita jana wameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya ushahidi uliotolewa na Jamhuri kuwa na utata.
Hakimu aliyekuwa akisoma hukumu kwenye kesi hiyo ya uhujumu uchumi Dkt Patricia Kisinda, amesema mbali na sababu hizo, Mahakama imegundua kuwa hati ya mashitaka ilikuwa na mapungufu na kuwa ushahidi uliotolewa dhidi yao mahakamani hapo haujathibitishwa.
Sabaya ameshinda kesi ya pili iliyokuwa inamkabili ambayo ilihusu tuhuma za uhujumu uchumi wakidaiwa kuchukua milioni 90 za Mfanyabiashara wa Arusha Francis Mrosso.
Washtakiwa walioachiwa huru leo pamoja na Sabaya ni Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.