Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema waliokuwa Makatibu Wakuu wa wizara, Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa mikoa na wilaya, wanaendelea kulipwa mishahara na marupurupi wanayolipwa warithi wao na hivyo kuibebesha mzigo Serikali.
Kauli hiyo ameitoa leo Jumanne Juni 14, 2022 bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha akiwasilisha bungeni mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mwigulu amependekeza kurejeshwa kwa watatumishi hao kwenye nafasi zao za awali kabla hawajapandishwa.
“Napendekeza yeyote aliyetokea kwenye nafasi yake ya kuteuliwa akitolewa akabaki kwenye utumishi wa umma arejee pia kwenye mshahara wake wa zamani ili kuwapunguzia watanzania mzigo wa kuwalipa watu waliokaa benchi huku wakiziba nafasi za vijana wapya kuajiriwa,” amesema.
Amesema unaweza kukuta nchi ina Wizara 25 ila ina Makatibu Wakuu 50 au zaidi, au Halmashauri 184 lakini kuna wakurugenzi 300 au zaidi na hivyo hivyo kwa nafasi nyingine. Wengine wamesabaisha upotevu na hasara kwa Taifa,
“Wote wanaendelea kuwabebesha mzigo Watanzania na wanaziba nafasi ya ajira mpya kwa vijana kwa kulipwa mshahara wa nafasi walizotolewa.mambo haya hayavutii lakini lazima tuambizane ukweli.
“Rais Samia Suluhu Hassan, anakerwa kuona fedha nyingi zinakwenda kwenye matumizi ya kawaida,” amesema.