Wabunge wataka uchunguzi hujuma Bwawa la Nyerere



 
MBUNGE wa Viti Maalum, Halima Mdee, ameitaka serikali kutoa maelezo kuhusu Sh. trilioni 6.5 ambazo analipwa mkandarasi anayejenga bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere.

Amesema kuwa katika hilo, pia anahitaji kujua kiasi ambacho nchi inalipwa kutokana na uzembe alioufanya wa kuchelewesha kukamilisha mradi huo kwa mujibu wa mkataba.

Mdee aliyasema hayo jana bungeni jijini hapo alipochangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Alisema anataka kujua nchi inapata nini kutokana na uzembe huo ili wajue kama bado kuna shida ya mikataba na wanasheria hawajajifunza kutokana na makosa.

"Katika mradi ambao serikali imewekeza kwa asilimia 100 ni Bwana la Mwalimu Nyerere, fedha za ndani za mradi huu ni Sh. trilioni 6.5, ulitakiwa kukamilika Juni 14, leo tunaambiwa umefikia asilimia 57.


 
"Tunajua kwenye mkataba kuna sura mbili, Mwanasheria Mkuu yupo hapa, upande mmoja ukiwa na uzembe upande mwingine lazima ufidiwe, ninakuomba waziri ukija kutujibu hapa utuambie hasara ambayo Tanzania imepata kwa mkandarasi huyu kutomaliza Juni 14 tunalipwa kiwango gani?" Alihoji.

Mbunge huyo alisema amesoma taarifa ya kamati ya sasa na ya mwezi Februari na kuona zinatofautiana.

"Mwezi wa pili Kamati ya Nishati na Madini imeeleza sababu tisa za msingi, hizo sababu tisa ni za uzembe wa mkandarasi, leo wanatuambia ni UVIKO-19 wakati Mheshimiwa Naibu Waziri ninakumbuka ulikuja katika Kamati ya Bajeti ukatuambia mkandarasi amesema UVIKO-19 lakini nyie kama serikali mmegundua tatizo siyo UVIKO-19 ila mkandarasi alikosea, alitakiwa ajenge matuta mawili lakini akajenga tuta moja wakati wa mafuriko ukavurugika," alisema.


"Haiwezekani kila siku tunapigwa, leo tunampa mtu kazi tena tunamlipa vizuri, kama kuna mtu analipwa kiroho safi ni huyu jamaa, hana hata stress (msongo wa mawazo), ninataka huyu anayekula fedha zetu bila msongo wa mawazo hajamaliza ujenzi kama mkataba unavyotaka, sababu zake alizotoa ni za uongo, waziri ulikuja hapa ukatuambia subiri mwezi wa sita si bado, mwezi wa sita ndio huu," alisema.

Mbunge huyo alimwomba waziri atoe majibu kuhusiana na suala hilo, akisema: "Kiroho safi, sina bifu na nyie, wote tunajenga nyumba moja, kiroho safi Sh. trilioni 6.5 ambazo tumempa huyu kwa heshima kubwa nchi inapata nini kutokana na uzembe? Ili tujue kumbe bado tuna shida ya mikataba, ili tujue wanasheria wetu bado hawajajifunza kutokana na makosa.

Mdee pia alihoji kuhusu mkataba ulioingiwa baina ya Shirika la Umeme (TANESCO) na Symbion ambayo sasa serikali inatakiwa kulipa Sh. bilioni 355 na kuhoji wanasheria walikuwa wapi.

Alimtaka waziri aeleze waliohusika wanawajibika kiasi gani na hatua zilizochukuliwa, akisema: "Baada ya kusema haya sina mengi sana, hayo mawili tu, nipate majibu kwa nia njema, nisipojibiwa tutakamata shilingi tu ili tujiachie zaidi."
Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumalizia Bwawa la Mwalimu Nyerere.


 
"Nina hofu ambayo sijui ninaogopa nini Kituo cha Msamvu kimeungua mara mbili ambacho ndicho kinalisha Bwawa la Nyerere, ninajiuliza ni hujuma au uzembe, wekeni kitengo cha uchunguzi ili kisiungue tena mara ya tatu," alisema.

Mbunge wa Lulindi, Issa Mchungahewa, alisema fedha zimewekwa kwenye mradi huo lakini hadi sasa haujakamilika ilhali ulitakiwa uwe umefika asilimia 98 ya ujenzi wake.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad