Wizara ya Afya imetoa taarifa kuhusu mwenendo wa UVIKO – 19 katika kipindi cha kuanzia Mei 05 hadi tarehe 03 mwezi huu inayoonyesha kuwa katika kipindi hicho kumekuwa na maambukizi mapya 161 ikilinganishwa na maambukizi 68 kwa kipindi cha kuanzia Aprili 02 hadi Mei 04 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt.Aifello Sichwale, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 137 na kwamba katika kipindi cha miezi miwili mfululizo kati ya Aprili hadi sasa hakuna kifo kilichoripotiwa.
Wagonjwa waliothibitika kuambukizwa UVIKO -19 katika kipindi cha kati ya Mei 05 na tarehe 03 mwezi huu wanatoka mikoa ya Dar es Salaam (130), Arusha (10), Mwanza (5), Shinyanga (4), Mtwara (3), Dodoma (2), Mara (2), Morogoro (1), Simiyu (1), Katavi (1), Kilimanjaro (1) na Mbeya (1).