Wanaoishi milimani Mwanza kuondolewa



 
WAKAZI wa Jiji la Mwanza waliojenga maeneo ya milimani wanatarajiwa kuondolewa ili kupisha wawekezaji kutoka nchini Brazil.

Wawekezaji hao wanatarajia kuwekeza kwenye sekta ya miundombinu, viwanda na utalii katika maeneo ya Igogo, Isamilo na Kegeto.

Akizungumza na Nipashe ofisini kwake hivi karibuni, Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine, alisema mpango huo unalenga kuboresha miundombinu pamoja na kukuza sekta ya utalii utakaogharimu Sh. bilioni 150.

Alisema makubaliano hayo yanahusisha wawekezaji kutoka nchini Brazil katika Jiji la Rio de Janeiro, ambao walifika jijini humo, kuangalia fursa za uwekezaji katika miundombinu, viwanda na utalii.

Costantine alisema maeneo mengine ambayo wawekezaji hao wanayalenga ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha pembejeo za kilimo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Kanda ya Ziwa.


 
“Sehemu zingine ni ujenzi wa barabara pamoja na nyumba za ghorofa katika milima mbalimbali ambayo inaangalia ufukwe wa Ziwa Victoria,” alisema.

Alitaja sehemu zingine watakazozigusa kuwa ni pamoja na kutengeneza eneo la ufukwe wa Ziwa Victoria sehemu ya kliniki, Nera jirani na kituo cha polisi wa majini ambalo litatengenezwa na kuwa sehemu za uwekezaji na utalii.

Constantine alisema mpango huo utasaidia ukuaji wa uchumi wa Jiji la Mwanza na mtu mmoja mmoja.


Alisema wawekezaji hao wana umoja wao nchini Brazil unaojulikana kama ‘Africa Unity’ na mpaka sasa wamewekeza nchini Dubai na Ethiopia.

Aliongeza kuwa katika makubaliano ya mpango huo, Jiji la Mwanza litatoa ardhi na wawekezaji watatoa mtaji, teknolojia na mradi huo utakapokamilika utanufaisha pande zote mbili.

ULIPAJI FIDIA

Akizungumzia uwekezaji wa maeneo ya milimani, Constantine alisema, jiji limepewa jukumu la kulipa fidia katika maeneo ya Igogo, Isamilo na Kegoto ambayo yapo mlimani ili kupisha uwekezaji huo.

Constantine alisema wawekezaji hao wamekubaliana na jiji litafute ardhi na kukamilisha mipango yote ndani ya miezi mitatu kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu kabla ya kazi hiyo kuanza.


 
Aliongeza kuwa wawekezaji hao wanaendelea kutafuta maeneo mengine ya kuwekeza ikiwamo mikoa ya Dodoma na Arusha.


 


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad