Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa ameagiza watendaji wa wizara wajipange kuhakikisha makosa yaliyojitokeza katika mgawanyo wa mirabaha hayajirudii tena.
“Yalijitokeza malalamiko mengi kutoka kwa wasanii na wadau mbali mbali juu ya mgawanyo wa Mirabaha. Nimewaagiza watendaji wa Wizara wajipange ipasavyo kuhakikisha kuwa malalamiko yaliyojitokeza hayajirudii tena katika mgao unaofuata.” amesema Waziri Mohammed Mchengerwa wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo leo Bungeni.
Aidha Wizara hiyo kwa kushirikiana na COSOTA imesema kwa sasa iko katika hatua ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu utakaowananufaisha wasanii na kazi zao za sanaa.
“Katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu juu ya malalamiko ya mgawanyo wa Mirabaha, Wizara na COSOTA tuko katika hatua ya kutafuta mwekezaji ambaye atawekeza katika mfumo wa kisasa utakaotoa taarifa jinsi kazi ya Muziki itakavyotumika katika vyombo vya habari, kwa ajili ya kubaini kiasi gani kinapaswa kukusanywa kwa wasanii kutoka kwenye vyombo hivyo.” Waziri Mchengerwa.