MABAO mawili ya Fiston Mayele na moja la Chiko Ushindi yametosha kwa Yanga kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara 28.
MABAO mawili ya Fiston Mayele na moja la Chiko Ushindi yametosha kwa Yanga kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Baada ya ukame wa misimu minne huku watani zao, Simba wakitwaa taji hilo mfululizo, Yanga imezinduka msimu huu na kutwaa kwa mara ya 28.
Shukrani za kipekee kwa mashabiki wa Yanga zimeelekezwa kwa Mayele usiku wa leo maana mbali na kupachika mabao hayo alitia asisti kwa Chiko aliyefunga bao lake la kwanza kwenye ligi tangu ajiunge na Yanga akitokea TP Mazembe.
Mayele alianza kupachika bao la kwanza kwenye mchezo huo dakika ya 34 kabla ya kumtengenezea Chiko na kupiga la ushindi kipindi cha pili.
Mabao mawili ambayo Mayele ametupia yanamfanya kurejea kwenye kilele cha wafumania nyavu Ligi Kuu Bara huku akimpiku bao moja mzawa, George Mpole mwenye mabao 15.
Awali Mpole alikuwa akiongoza orodha hiyo kwa tofauti ya bao moja kufuatia kupachika kwake bao kwenye mchezo uliopita wa Geita Gold dhidi Dodoma Jiji.
Ushindi huo unamaana kuwa Yanga imefikisha pointi 67 ambazo hakuna timu ambayo inaweza kuzifikia kwenye mchezo iliyosalia.
Licha ya Coastal kugeuzwa ngazi na Yanga kwenye mchezo huu inanafasi ya kulipiza kisasi kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la ASFC ambao watakutana.