Walinzi wasimulia padri aliyeuawa ippmedia.com



 
SIKU moja baada ya mwili wa Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya wa Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers), Michael Samson (63), kuokotwa akiwa amefariki, walinzi wa kituo alichokuwa akihudumia wameeleza namna alivyowaaga kabla ya kufikwa na umauti.

Padri Michael alikutwa amefariki kwenye Mto Meta chini ya Daraja la Sabasaba jijini hapa, huku mwili wake ukiwa umekatwa viungo na kutenganishwa.

Akizungumza na Nipashe mmoja wa walinzi wa Kituo cha Vijana cha Kanisa Katoliki Mbeya alikokuwa akiishi, Theresia Mwela, alisema Padri Michael ndiye aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo hicho na walikuwa wanaishi naye vizuri muda wote na hakuwahi kuwa na tatizo lolote.

Alisema kiongozi huyo alikuwa na utaratibu wa kuaga kila siku jioni akiwaeleza kuwa anakwenda kufanya mazoezi ya kutembea na kila baada ya mazoezi alikuwa akirejea na kutoa taarifa kuwa amerudi.

Mwela alisema kuwa siku ya Ijumaa alipoondoka kwa mara ya mwisho alitoa taarifa, lakini walishangaa kutorejea kama ilivyo kawaida yake mpaka siku iliyofuata walipopata taarifa kuwa mwili wake umeokotwa chini ya daraja ukiwa umecharangwa mapanga.


 
“Father mwenzake aliyekuwa anakaa naye alikuja na gari akasema anamtafuta hamuoni na mimi nikamweleza kwamba hajarudi, baada ya hapo aliondoka lakini kesho yake akaja akatuambia kwamba Father Samson ametutoka,” alisema Mwela.

Alisema pamoja na kuwa kiongozi Mkuu wa Kituo hicho, alikuwa mtu wa kujishusha na kuwasalimia watu wote wanaofanya kazi kituoni hapo.

Mwela alisema kiongozi huyo alikuwa mstaarabu na hakuwahi kuwa na makundi ya aina yoyote ambayo pengine yangehisiwa kuwa ni hatari kwa maisha yake.


Hata hivyo, uongozi wa kanisa hilo haukupatikana kutoa taarifa ya utaratibu wa mazishi ya Padri Michael, huku taarifa zikieleza kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya, Gervas Nyaisonga alikuwa safarini.

Juzi Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Ulrich Matei, lilitoa taarifa kuwa linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na kujua chanzo cha mauaji hayo, huku likilaani mauaji hayo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad