YANGA kuna moto unaendelea wa usajili na hawapoi. Wakimaliza kule wanawasha huku, injinia Hersi Said ametua nchini juzi alfajiri na haraka akamaliza usajili wa staa mmoja Mzambia.
Yanga imemsainisha mkataba wa mwaka mmoja mshambuliaji Lazarous Kambole raia wa Zambia ambaye muda mrefu walikuwa wakimpigia hesabu lakini dili likikwama.
Kambole amesaini mkataba haraka mbele ya Rais mtarajiwa wa Yanga injinia Hersi Said ukiwa ni usajili mwingine mkubwa ndani ya siku nne.
Mapema Hersi aliziliza klabu za Afrika Kaskazini na Simba akimsainisha mshambuliaji Stephan Aziz KI raia wa Burkina Faso na kuzima ubishi wa usajili staa huyo anayemalizia msimu na ASEC Mimosas ya nchini humo.
Wafadhili wa Yanga, GSM wamedhamiria kusuka kikosi chao bora kwa msimu ujao na watakuwa wakirejea kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kambole anaweza kutua nchini haraka Jumanne kuja kumaliza kila kitu na mabosi wa GSM na atakaa kwenye kochi jeupe kulamba dili hilo.
Kambole anakuja kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Yanga, huku klabu yake ya mwisho kuitumikia ikiwa ni Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ambayo alimalizia mkataba wake msimu huu.
Hata hivyo, Yanga itahitaji Kambole aje ajipange upya msimu ujao akiwa na klabu yao kutokana na muda mrefu amekuwa sio chaguo la kwanza ndani ya Chiefs maarufu kwa jina la Amakhosi.
Usajili huo unaifanya sasa Yanga kuwa na mashine tatu za kusumbua katika safu yao ya ushambuliaji kwa msimu ujao akiwemo mfungaji wao bora msimu huu staa Fiston Mayele, Kambole na KI.
Usajili huo unaiweka katika wakati mgumu nafasi ya Mkongomani Heritier Makambo ambaye ameshindwa kuonyesha moto wake ndani ya klabu hiyo akifunga jumla ya mabao manne kwenye mashindano yote, matatu katika Kombe la Azam Shirikisho na moja kwenye ligi.