WAKATI wakiwa katika pilika za uchaguzi Mkuu, uongozi wa klabu ya Yanga umeamua kufunga safari kwenda nchini Ivory Coast kumfuata kiungo wa ASEC Mimosas, Stephan Aziz Ki kwa ajili kumsajili ili aitumikie timu hiyo msimu ujao.
Katika kuhakikisha usajili huo unafanikiwa, Makamu Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Injinia Hersi Said ametua nchini Ivory Coast kwa ajili ya kukamilisha dili la nyota huyo.
Kutokana na safari hiyo, Hersi fomu yake ya kuwania nafasi ya urais kwenye Klabu ya Yanga ilirudishwa na mzee Mohammed Msumi, Juni 9 mwaka huu, wakati yeye akiwa kwenye majukumu ya usajili.
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka ndani ya Yanga, Hersi yupo nchini Ivory Coast kuhakikisha wanamaliza na na mchezaji huyo ambaye ametengewa dola elfu 5,000 (sawa na Shilingi 11,650,000) kama mshahara wake wa mwezi.
“Sasa hivi tunafanya usajili kulingana na michuano iliyopo mbele yetu, msimu uliopita hatukufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika na tulitolewa mapema, safari hii hatutaki kurudia makosa hayo ndio maana unaona Hersi ameondoka nchini kwenda kumalizana na Aziz Ki kule nchini Ivory Coast,” kilisema chanzo chetu.
Alisema baada ya kufanya mazungumzo na Wakala wa mchezaji huyo alimueleza Hersi kwamba, anatakiwa kukutana na nyota huyo baada ya kumaliza majukumu ya timu yake ba timu ya taifa katika mashindano ya kufuzu AFCON.
Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingiza alisema msimu huu wamejipanga kuimarisha kikosi chao kwa kufanya usajili mzuri kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Nesredine Nabi.
“Kuhusu Fiston Mayele ataendelea kubaki ndani ya Yanga ili kuhakikisha tunafanya usajili kulingana na mashindano yaliyopo mbele yetu,” alisema Senzo.