Yanga shangwe Mbeya, Simba ikimnasa Mpole



WAKATI mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wanatarajiwa kuwakabili wenyeji Mbeya City katika mechi ya raundi ya 29 itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Simba imefanikiwa kunasa saini ya straika wa Geita Gold FC, George Mpole.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema mechi hiyo itakuwa ngumu kwa sababu wenyeji wao wanakikosi imara, lakini wamejiandaa kupata matokeo mazuri.

Hata hivyo Nabi alisema wachezaji wake wanakabiliwa na uchovu kutokana na kucheza mechi mfululizo.

"Tunategemea mchezo utakuwa mgumu, lakini tumejiandaa na matokeo mazuri, tumecheza mechi mfululizo, kila baada ya siku mbili tunacheza, kwa hiyo kuna mchoko kwa wachezaji wangu, wanahitaji muda wa kupumzika pamoja na yote haya, lakini tuko makini," alisema Nabi.

Aliongeza mchezaji pekee ambaye ana uhakika ataukosa mchezo huo ni Mkongomani Chiko Ushindi kutokana na majeraha.


 
Mbali na Yanga kuwa tayari imeshatwaa ubingwa wa msimu huu, lakini mechi hiyo itakuwa muhimu katika kuendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi hata moja.

Pia ni moja kati ya mechi ambazo zinaweza kumfanya straika wao, Fiston Mayele kupachika mabao katika harakati zake za kutaka kutwaa kiatu cha dhahabu huku wakibakiza mechi moja ambayo ni dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa Juni 29, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Viongozi na wadau mbalimbali wa Yanga, wako Mbeya kwa ajili ya sherehe hizo na baada ya hapo wanatarajiwa kusafiri kurejea Dar es Salaam na kupata mapokezi makubwa.


Taarifa za uhakika kutoka Simba zinasema tayari Mpole pamoja na winga wa Kagera Sugar, Nassoro Kapama wamesaini mkataba wa miaka miwili kila mmoja.

Nipashe liliwasiana na nyota hao, Mpole na Kapama ambapo walikiri kufuatwa na klabu kongwe hapa nchini na kuhakikisha kwamba baada ya msimu huu kufikia tamati wataweka wazi mipango yao.

“Ni kweli Simba na Yanga zilileta ofa zao ila ni wapi nitakwenda ni suala la muda ukifika litawekwa wazi kama ni Simba kama inavyotajwa tutajua baadaye,” alisema Mpole.

Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema ni kuhusu suala ya usajili kuna baadhi ya wachezaji wameshamalizana na kinachosubiriwa utambulisho.


 
"Usajili umekamilika kwa asilimi kubwa tumesajili vyuma vya hatari, kuhusu Okrah (Augustine), ni hatari anapiga mashuti balaa, mchakato wa kujiunga na Simba ni suala la muda," alisema Ahmed.

Aliongeza viongozi wa Simba wanafanya usajili kulingana na mahitaji ya kikosi chao na sio kwa sifa za kupiga picha na wachezaji ambao bado hawajasaini mkataba kwa ajili ya sifa.

"Tunafanya usajili kulingana na mapungufu yetu ya msimu huu, tunakubali tumepoteza lakini usajili tunaofanya msimu huu ni kabambe," Ahmed aliongeza.

Mshambuliaji wa Backem United ya Ghana, Okrah ni mmoja wa nyota wanaotajwa kuwindwa ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi na kilichobakia ni muda kuzungumza.


Naye Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Selemani Matola akizungumzia mchezo wa juzi na Mtibwa Sugar alisema ulikuwa mgumu na amewapongeza wachezaji wake kufuata maelekezo na kufanikiwa kupata pointi tatu muhimu na kuwapa furaha mashabiki wao.

Kuelekea mechi dhidi ya Tanzania Prisons itakayochezwa kesho, Matola alisema watapambana kuhakikisha wanapata pointi zote sita kumaliza vizuri msimu kwa heshima.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad